Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lampongeza Ndejembi kuteuliwa Makamu wa Rais
Na. Coletha Charles, DODOMA
Baraza
la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limempongeza Waziri wa Nishati na
Mbunge wa Jimbo la Chamwino, Deogratius Ndejembi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) tarehe 26 Agosti 2026.
Pongezi hizo zilitolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bakari Fundikira wakati akiongoza Baraza maalum la Madiwani kwa ajili ya kupokea taarifa ya ufungaji wa hesabu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Fundikira
alisema kuwa Baraza zima la Madiwani linampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua Deogratius Ndejembi
kushika nafasi hiyo ya Makamu wa Rais, huku akimtakiwa heri katika utekelezaji
wa majukumu yake mapya.
“Lakini
pia tutumie nafasi hii kumpongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi
alioufanya wa kumteua ndugu yetu Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, Baraza zima la Madiwani linampongeza
sana,” alisema Fundikira.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Zuzu, Jenesta Malingo alisema kuwa uteuzi wa
Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais ni hatua muhimu inayopaswa kupongezwa,
akieleza kuwa nafasi hiyo inaonesha imani aliyopewa na Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kuendelea kulitumikia taifa.
“Uteuzi
wa mheshimiwa Ndejembi kuwa Makamu wa Rais ni jambo kubwa na la kujivunia.
Tunampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa nafasi hii,
na tunamtakia mheshimiwa Ndejembi kila la heri katika majukumu yake mapya ya
kulitumikia taifa,” alisema Malingo.
Uteuzi huo ulitangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, Agosti 26, 2026 katika Ofisi Ndogo za CCM, Lumumba, Dar es Salaam, baada ya Ndejembi kupendekezwa kuchukua nafasi ya Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyejiuzulu. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimthibitisha Agosti 28, 2026 kwa kura 324 sawa na asilimia 100 huku hatua inayofuata ikiwa ni kuapishwa rasmi kabla ya kuanza majukumu yake mapya ya Umakamu wa Rais.
Comments
Post a Comment