Usafi wa Jumamosi, ni usafi wa kila siku

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesisitiza wananchi kuacha dhana kwamba usafi wa mazingira ni jukumu la kufanyika siku ya Jumamosi pekee, akieleza kuwa usafi ni wajibu wa kila mwananchi na unapaswa kufanyika kila siku.

 


Senyamule alitoa kauli hiyo jana wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini hapa, kilichowakutanisha maafisa watendaji wa kata, mitaa, wenyeviti wa mitaa, maafisa afya na maafisa mazingira kutoka Jiji la Dodoma, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu umuhimu wa kuhakikisha miji na maeneo ya makazi yanakuwa safi.

Akizungumza katika kikao hicho, mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa utaratibu wa kufanya usafi wa mazingira kila Jumamosi umefutwa, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuufanya usafi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.

“Nimefuta utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi. Watu wafungue shughuli zao kuanzia mapema asubuhi,” alisema Senyamule.

Aidha, aliwaagiza maafisa watendaji wa kata, mitaa na maafisa afya kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa usafi wa mazingira kila siku, ikiwemo siku za Jumamosi na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya watu wanaokiuka sheria na taratibu za usafi wa mazingira.

Alisema kuwa Mkoa wa Dodoma umejipanga kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa, ikiwemo kuhakikisha usimamizi mzuri wa maji taka na maeneo yanayoweza kuwa hatarishi.

Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari, kuzingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka pamoja na kushirikiana na viongozi katika kuhakikisha mifumo ya maji taka na mazingira kwa ujumla inasimamiwa ipasavyo.

Kikao kazi hicho ni sehemu ya juhudi za mkoa na Halmashauri za Dodoma kuimarisha usafi wa mazingira na utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhusu usafi wa miji, kwa lengo la kulinda afya za wananchi na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na bora kwa maisha ya kila siku.

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha taarifa ya ufungaji hesabu 2025/2026

Wilaya ya Dodoma kuchanja watoto zaidi ya laki 2 chanjo ya Polio

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lampongeza Ndejembi kuteuliwa Makamu wa Rais