Ukaguzi wa watumishi Kanda Namba Sita walenga kuboresha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali watu
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Zoezi la ukaguzi wa watumishi katika vituo vya kazi
limefanyika katika Kanda Namba Sita, likilenga kuhakikisha uwepo wa taarifa
sahihi za watumishi, kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili, pamoja na
kuwakumbusha kuhusu umuhimu wa kujaza mfumo wa PEPMIS.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Afisa Utumishi Kanda, Jane Mwagalaba, alisema kuwa ukaguzi huo unahusisha kutembelea vituo vya kazi ili kuhakiki uwepo wa watumishi, kusikiliza changamoto zao na kupokea maoni yanayoweza kusaidia kuboresha mazingira ya kazi.
“Zoezi hili linahusu ukaguzi wa watumishi katika vituo vya kazi, kusikiliza changamoto zao, kuchukua maoni, lakini pia kuwasisitiza kuhusu ujazaji wa PEPMIS,” alisema Mwagalaba.
Alisema kuwa moja ya malengo makuu ya zoezi hilo ni kuwa na data sahihi za watumishi katika vituo vyao vya kazi, jambo ambalo ni muhimu katika kupanga na kusimamia rasilimali watu kwa ufanisi.
Katika awamu ya kwanza, alisema kuwa zoezi hilo limewalenga walimu wa shule za msingi na sekondari katika Kanda Namba Sita, ambapo jumla ya shule 13 zimefanyiwa ukaguzi.
Zoezi hilo linatarajiwa kusaidia kuboresha usimamizi
wa watumishi, upatikanaji wa taarifa sahihi za kiutumishi na kuongeza uelewa wa
watumishi kuhusu wajibu na masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wao.
Zoezi hilo ni endelevu na linaweka msisitizo katika matumizi sahihi ya mifumo ya kiutumishi, ikiwemo PEPMIS, ili kuwezesha taarifa za watumishi kuwa sahihi na kutumika katika kufanya maamuzi yenye tija katika usimamizi wa rasilimali watu.
Comments
Post a Comment