LAAC yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo jijini Dodoma
Na. Jesca Kipingu, DODOMA
Kamati
ya Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa (LAAC) imeridhishwa na utekelezaji wa
miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, huku
ikipongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri kuhakikisha miradi hiyo
inatekelezwa kwa kuzingatia ubora, thamani ya fedha na mahitaji ya wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Abdallah Chikota, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ikiwemo ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.6 inayoelekea Hospitali ya Jiji la Dodoma katika eneo la Nala pamoja na ujenzi wa jengo jumuishi katika Kituo cha Afya Makole, ambalo linajengwa kwa mfumo wa ghorofa.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, Chikota aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
namna inavyotekeleza miradi hiyo, akieleza kuwa kamati imeridhishwa na matumizi
ya fedha pamoja na ubora wa kazi zinazofanyika.
“Tunawapongeza
kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo ambao umezingatia thamani ya fedha
iliyotumika. Kwa upande wa barabara, mmejenga kwa kiwango kizuri na cha ubora,
huku katika Kituo cha Afya Makole mmeonesha ubunifu mkubwa. Kutokana na ufinyu
wa eneo, badala ya kujenga majengo ya kawaida ya chini, mmejenga jengo la
ghorofa ambalo linaongeza uwezo wa kituo kutoa huduma na hatimaye kukifanya
kiwe na hadhi ya hospitali,” alisema Chikota.
Aidha,
Chikota alieleza kuwa utekelezaji wa miradi yenye ubora na inayozingatia
thamani ya fedha una mchango mkubwa katika kuhakikisha rasilimali za umma
zinatumika kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma bora. Alisisitiza umuhimu wa
Halmashauri kuendelea kusimamia miradi kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika
kwa wakati na inaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Awali,
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma, Vincent Odero, alisema ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kuelekea
Hospitali ya Jiji la Dodoma – Nala umegharimu Shilingi bilioni 2.874. Alisema
mradi huo unalenga kurahisisha usafiri na kuwawezesha wananchi kufika
hospitalini kwa urahisi, pamoja na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za
afya katika eneo hilo.
Huku ujenzi wa jengo jumuishi la kutolea huduma
katika Kituo cha Afya Makole, Odero alisema mradi huo utakapokamilika
utagharimu takribani Shilingi bilioni 6.9, ambazo zinatokana na fedha kutoka
Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Ziara
hiyo ya Kamati ya Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa (LAAC) inalenga
kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri, kujiridhisha
kuhusu matumizi sahihi ya fedha za umma, ubora wa miradi na uzingatiaji wa
sheria, kanuni, taratibu na viwango vinavyotakiwa katika utekelezaji wa miradi.
Comments
Post a Comment