Dodoma yaweka mkakati wa kuimarisha usafi wa Mazingira

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu amewataka watendaji wa kata na mitaa kusimamia ipasavyo usafi wa mazingira na kuhakikisha sheria ndogo zinazohusu udhibiti wa wanyama zinafuatwa, ili kudhibiti ongezeko la wanyama wanaozurura katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.

 


Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya jiji la Dodoma uliopo Mji wa Mtumba, jijini Dodoma, aliwasisitiza umuhimu wa watendaji kujipanga kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa za El Niño, kwa kuandaa mipango ya kukabiliana na athari zake kuanzia ngazi ya kata hadi mtaa.

Aliwataka watendaji kutumia mamlaka walizonazo katika kuchukua hatua stahiki pindi wanapobaini ukiukwaji wa sheria na taratibu za usafi na mazingira.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi aliwataka watumishi kuwa na utayari wa kuchukua hatua katika utekelezaji wa majukumu yao, badala ya kusubiri maelekezo katika kila jambo.

 



Aliishauri halmashauri kuangalia uwezekano wa kuweka motisha kwa watumishi wanaofanya vizuri katika kusimamia usafi wa mazingira, hatua ambayo inaweza kuongeza ari na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Nae, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Vincent Odero aliwataka wenyeviti wa mitaa kutoa ushirikiano kwa maafisa watendaji katika kusimamia usafi wa mazingira na kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi wakati wote.

Alieleza kuwa maafisa mazingira wataendelea kupimwa kwa kuzingatia namna wanavyosimamia usafi katika maeneo yao, huku akieleza kuwa jiji linaendelea na maandalizi ya kuhusisha makampuni katika ukusanyaji wa taka ngumu.




Aidha, alisema kuwa jiji linaendelea kuimarisha udhibiti wa ujenzi ili kuhakikisha shughuli za ujenzi zinafanyika kwa utaratibu unaozingatia mipango ya mji na mazingira bora kwa wananchi.

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha taarifa ya ufungaji hesabu 2025/2026

Wilaya ya Dodoma kuchanja watoto zaidi ya laki 2 chanjo ya Polio

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lampongeza Ndejembi kuteuliwa Makamu wa Rais