RC Kheri James: Elimu iwe silaha yenu dhidi ya rushwa
Na. Muhamad Said, IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James
amewataka wanafunzi wa klabu za wapinga rushwa kutoka mikoa ya Iringa na Dodoma
kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa, akisisitiza kuwa elimu
na uadilifu ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.
Akizungumza katika mdahalo wa klabu za wapinga rushwa za shule za msingi na sekondari unaofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Lugalo, amewahimiza wanafunzi kutambua madhara ya rushwa na kuanza mapema kujenga utamaduni wa kuikataa, akieleza kuwa kizazi cha leo ndicho kitakachobeba dhamana ya uongozi na maendeleo ya taifa hapo baadaye.
Alisisitiza kuwa suala la kupinga rushwa
linapaswa kupigwa vita na watu wote wakiwemo wanafunzi, akiongeza kuwa vijana
wanapaswa kuwa mabalozi wa uadilifu katika shule zao, familia na jamii kwa
ujumla kwa kukataa vitendo vya rushwa na kuhamasisha wenzao kusimamia haki na
uwajibikaji.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka
wanafunzi kutumia midahalo kama fursa ya kujenga maarifa, kujiamini na kubadilishana
mawazo, badala ya kuiona kama uwanja wa kushindana kwa namna inayoweza kuwagawa
akisema kuwa ushindani unaofaa katika midahalo ni ule unaojenga uwezo wa
kufikiri, kujenga hoja na kujifunza kutoka kwa wengine.
“Msishindane kwa lengo la kumshinda mwenzenu tu, shindaneni kwa lengo la kujifunza, kubadilishana maarifa na kujenga uwezo wa kufikiri. Mshindi wa kweli ni yule anayepata maarifa zaidi” alisema Kheri.
Alihitimisha kwa kusema kuwa taifa linahitaji kizazi cha vijana wenye maarifa na misingi imara ya maadili ambao watakapokuwa viongozi, wataalamu na watendaji katika sekta mbalimbali watasimamia rasilimali za nchi kwa uaminifu na kuweka mbele maslahi ya watanzania.
Comments
Post a Comment