LAAC yalipongeza Jiji la Dodoma kwa ubunifu wa Jengo Jumuishi Kituo cha Afya Makole
Na. Mwandishi Wetu, VIWANDANI
Halmshauri ya Jiji la Dodoma imepongezwa na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa ubunifu wa kujenga
jengo jumuishi la huduma za afya la ghorofa tatu katika Kituo cha Afya Makole lenye gharama ya shilingi
bilioni 6.9 hatua inayolenga kutatua changamoto ya uhaba wa eneo na kukidhi
ongezeko la mahitaji ya huduma za afya katika jiji hilo.
Pongezi hizo zilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa (LAAC), Abdallah Chikota wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo Kata ya Viwandani Jiji la Dodoma.
Chikota alisema kuwa mfumo wa kujenga ghorofa ulikuwa
ndio mbadala sahihi wa kukabiliana na changamoto ya uhaba wa eneo na kupanua
huduma za matibabu, bila kulazimika kutafuta eneo jipya nje ya kituo hicho cha
afya.
“Kwanza tunalipongeza Jiji la Dodoma kwa ubunifu wao
na mawazo ya kisasa kwa sababu hapa Kituo cha Afya Makole kuna changamoto ya
eneo, kwa hiyo ili kutatua tatizo hilo wameamua kujenga jengo la ghorofa tatu.
Jengo hili likikamilika tutakuwa na kituo cha hadhi ya juu katika jiji letu la
Dodoma,” alisema Chikota.
Aliongeza kuwa ubunifu huo ni muhimu zaidi kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma za afya katika Jiji la Dodoma, akibainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Makole kuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa hadhi ya hospitali ya jiji.
Akisoma taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji,
Vincent Odero, alisema kuwa mradi huo umechangiwa na uwekezaji unaohitajika
kutokana na ongezeko la idadi ya watu na mahitaji ya huduma za afya katika
Kituo cha Afya Makole, kilichopo katikati ya jiji.
Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanawake waliojifungua kwa njia ya kawaida iliongezeka kutoka 3,683 mwaka 2017 hadi 6,989 mwaka 2025, huku waliojifungua kwa njia ya upasuaji ikiongezeka kutoka 226 hadi 957 katika kipindi hicho.
Kwa ujumla, LAAC imeridhishwa na utekelezaji wa mradi
huo wa jengo jumuishi la huduma za afya katika Kituo cha Afya Makole,
unaotekelezwa kwa ushirikiano wa fedha kutoka serikali kuu pamoja na mapato ya
ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Comments
Post a Comment