Wananchi watakiwa kufanya usafi kila siku kuweka Dodoma safi
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Wananchi
na wafanyabiashara katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya
usafi kila siku katika maeneo yao badala ya kusubiri siku ya jumamosi ya mwisho
wa wiki ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, salama na rafiki kwa afya za
jamii.
Wito huo ulitolewa na Meneja Kanda Namba Moja, Nicholaus Mitembo mara baada ya kushiriki zoezi la usafi wa pamoja katika Soko la Miembeni Jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa usafi si jukumu la mamlaka pekee bali ni wajibu wa kila mwananchi na mfanyabiashara.
Alisema
kuwa msisitizo huo unatokana na kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Rosemary Senyamule katika kikao na Maafisa Mazingira pamoja na maafisa afya
ambapo alisisitiza kuwa kufanya usafi siku ya Jumamosi pekee haitoshi. “Usafi
wa Jumamosi pekee hautoshi. Kila mwananchi na mfanyabiashara ana wajibu wa
kushiriki katika usafi kila siku. Niwasihi wananchi wote pamoja na
wafanyabiashara tusisubiri siku ya Jumamosi pekee, bali tuwe tunafanya usafi
kila siku katika maeneo yetu ili kuhakikisha tunakuwa na mazingira safi na
salama,” alisema Mitembo.
Kwa
upande wake, mfanyabiashara wa Soko la Miembeni, Saida Shabani alisema kuwa
wana wajibu wa kuhakikisha maeneo ya biashara zao yanakuwa safi wakati wote
kwasababu mazingira safi ni sehemu muhimu ya kuwavutia wateja. “Tumefanya usafi
katika eneo letu hapa Korongoni, sokoni lakini naomba nitoe wito kwa
wafanyabiashara wenzangu tufanye usafi kila siku. Haya ndiyo maeneo yetu ya
kazi, hivyo tukiyaacha yakiwa machafu na mazingira yakiwa mabovu, wateja
hawatafika. Tujitahidi kufanya usafi kila siku katika maeneo yetu ya kazi
pamoja na maeneo yetu ya nyumbani” alisema Shabani.
Ushirikiano
wa wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika kuzingatia usafi wa
mazingira unatarajiwa kuendelea kuwa msingi wa kulifanya Jiji la Dodoma kuwa
safi, salama na lenye mazingira bora kwa wakazi, wafanyabiashara na wageni.
Comments
Post a Comment