RC Dodoma amtaka Mkandarasi kuongeza kasi ukarabati Soko la Majengo


Na. Mohammed Ramadhani,
MAJENGO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amemtaka mkandarasi anayetekeleza ukarabati wa Soko la Majengo jijini Dodoma kuongeza kasi ya kazi ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda wa nyongeza wa siku 60 uliotolewa.



Senyamule alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa Soko la Majengo, akieleza kuwa soko hilo lina mchango mkubwa katika kutoa huduma na kukidhi mahitaji ya wananchi wa Jiji la Dodoma.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa utekelezaji wa kazi unaelekea vizuri, lakini mkandarasi anapaswa kutumia kikamilifu muda wa nyongeza aliopewa ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati.

Aidha, alishauri kuwa mkandarasi kuongeza muda wa utekelezaji wa kazi kwa kufanya kazi hadi nyakati za usiku kwa kutumia taa, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.


Alisisitiza umuhimu wa kukamilisha kazi kabla ya kuanza kwa mvua, akieleza kuwa kuchelewa kwa utekelezaji kunaweza kuathiri kasi ya mradi na kuongeza changamoto katika kipindi cha mvua.

Soko la Majengo linatarajiwa kuwa sehemu muhimu katika utoaji wa huduma na mahitaji mbalimbali kwa wananchi wa Jiji la Dodoma, huku serikali ikiendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa.






Comments

Popular Posts

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Zoezi la Kuua Mbwa Wanao Zurura Lafanyika Kata ya Msalato

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira