Jiji la Dodoma laweka mkakati wa kudhibiti msongamano wa Bajaj na Daladala Stendi ya Mnada mpya
Na. Mwandishi wetu, KIZOTA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza kuchukua hatua
za kuboresha matumizi ya Kituo cha Mabasi Mnada Mpya kilichopo Kata ya Kizota
kwa kuhakikisha daladala na bajaji zinaingia ndani ya kituo hicho wakati wa
kupakia na kushusha abiria, badala ya kusimama nje ya kituo.
Hatua hiyo inalenga kuweka utaratibu katika eneo hilo, kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri pamoja na kuimarisha usalama na urahisi wa huduma kwa wananchi wanaotumia kituo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya
mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mnada Mpya iliyopo Kata ya Kizota, Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Rosemary Senyamule, alisisitiza umuhimu wa halmashauri kuhakikisha
kituo hicho kinatumika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
Senyamule alielekeza daladala na bajaji kuingia ndani
ya kituo wakati wa kupakia na kushusha abiria, akieleza kuwa hatua hiyo
itasaidia kuboresha mtiririko wa usafiri na kuhakikisha mazingira ya kituo
yanakuwa salama na yenye utaratibu.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa aliitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuendelea kusimamia kwa karibu changamoto za miundombinu zinazoweza kuathiri matumizi ya kituo hicho, ikiwemo hali ya barabara zinazoingia katika kituo hicho, pamoja na kuzingatia maandalizi ya kukabiliana na mvua zinazotarajiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt.
Frederick Sagamiko, alisema kuwa halmashauri imepokea maelekezo hayo na imeanza
kuchukua hatua kuhakikisha shughuli za usafiri katika Kituo cha Mnada Mpya
zinafanyika kwa utaratibu na wananchi wanapata huduma bora.
Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na
wadau wa usafiri pamoja na wananchi katika kuboresha matumizi ya kituo hicho na
kushughulikia changamoto zinazojitokeza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za
kuimarisha huduma za usafiri ndani ya Jiji la Dodoma.
Comments
Post a Comment