Teknolojia ya Kinengunengu mkombozi kwa vifaranga vya kuku Dodoma
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma limeibua ubunifu mpya wa teknolojia ya banda maalumu la
kufugia vifaranga vya kuku maarufu kama ‘Kinengunengu’ linalolenga kuwasaidia
wafugaji kupata njia bora ya kuwapatia vifaranga joto, chakula, malazi na
mazingira salama ya ukuaji.
Banda hilo limekuwa miongoni mwa vivutio vikubwa katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni kupitia banda la Jiji la Dodoma, ambapo wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kujifunza namna ya kuanza na kuendeleza ufugaji wa kuku kwa njia rahisi na salama.
Akielezea banda hilo, Afisa Mifugo wa Jiji la Dodoma, Delila Mlamka alisema kuwa wafugaji wengi wamekuwa wakitegemea matumizi ya taa na mkaa kwa ajili ya kuwapatia vifaranga joto, lakini teknolojia ya Kinengunengu imekuja kuondoa utegemezi huo kwa kutumia muundo unaoweza kuhifadhi joto ndani ya banda.
Alisema
kuwa Kinengunengu kimeundwa katika mfumo wenye sehemu mbili muhimu, sehemu ya
kulala ambayo huzibwa zaidi wakati wa usiku ili kuhifadhi joto, na sehemu ya
kula ambayo huwa wazi kwa juu na sehemu ya vifaranga hao kutumia mchana ili
kuruhusu upatikanaji wa chakula na hewa ya kutosha.
“Jiji la Dodoma limeunda Kinengunengu ili kuwapa wafugaji elimu ya vitendo kuhusu namna ya kuhudumia vifaranga katika hatua za mwanzo. Banda hili linasaidia kuhakikisha vifaranga wanapata joto linalohitajika, chakula, maji safi na mazingira yanayowalinda dhidi ya changamoto mbalimbali,” alisema Mlamka.
Aliongeza kuwa teknolojia hiyo inalenga kuwasaidia wafugaji kupunguza gharama za uzalishaji, hasa gharama za kununua mkaa au kutumia umeme kwa ajili ya taa za joto, huku ikisaidia pia kupunguza changamoto za vifo vya vifaranga vinavyosababishwa na baridi.
Kwa
upande wake mfugaji wa kuku kutoka Kata ya Nzuguni, jijini hapa, Prisca Chana
alisema kuwa banda hilo limeonesha kuwa ufugaji wa kisasa unaweza kuanza kwa
kutumia ubunifu unaopatikana ndani ya mazingira ya mfugaji.
“Kinachowafanya
vifaranga wakue vizuri ni kupata mazingira sahihi. Teknolojia hii imesaidia
kuonesha kuwa mfugaji anaweza kutunza joto bila kutegemea gharama kubwa za mkaa
au taa,” alisema Chana.
Nae,
mkazi wa Kata ya Nala, Julias Kesi anayetamani kuanza kufuga kuku lakini
anaishi kwenye nyumba ya kupanga alisema kuwa ubunifu huo umempa matumaini ya
kuanza ufugaji kwa kiwango kidogo.
“Changamoto
yangu ilikuwa nafasi na gharama za kuendesha ufugaji, lakini baada ya kuona
Kinengunengu nimegundua kuwa naweza kuanza na idadi ndogo ya vifaranga bila
kutumia vifaa vya gharama kubwa,” alisema Kesi.
Ubunifu
wa teknolojia ya Kinengunengu ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha ufugaji bora
wa kuku na kuwasaidia wananchi kuongeza kipato kupitia teknolojia rahisi, nafuu
na inayozingatia mahitaji ya vifaranga.
Comments
Post a Comment