Silage suluhisho la uhaba wa chakula cha ng'ombe Dodoma
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI
Wafugaji
wa ng’ombe katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamehimizwa kuanza kutengeneza
na kuhifadhi chakula cha mifugo kilichochachushwa (Silage) ili kuhakikisha
mifugo inapata lishe ya kutosha wakati wa kiangazi, kipindi ambacho maeneo
mengi hukumbwa na upungufu mkubwa wa malisho kutokana na ukame.
Rai hiyo ilitolewa na Afisa Mifugo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Delila Mlamka wakati akiwaelezea wananchi waliotembelea banda la mifugo la halmashauri hiyo katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini hapa.
Alisema
kuwa Silage ni chakula kinachotengenezwa kwa kuchanganya majani mabichi
yaliyokatwakatwa, kiasi kidogo cha majani makavu, pumba na molases, kisha kuhifadhiwa
kwenye mazingira yasiyoruhusu hewa ya oksijeni kuingia kwa siku 21 ili
kichachuke vizuri na kuwa salama kwa matumizi ya mifugo.
Alisema
kuwa chakula hicho kinaweza kutengenezwa
kwenye mashimo au mapipa na kuhifadhiwa katika mifuko midogo ya plastiki na
mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka ‘kinga njaa’, ila tu hewa isiingie ndani ya
kifungashio.
“Silage
ni lishe bora na kinapendwa sana na ng’ombe wa maziwa kwa sababu kina
mchanganyiko wa majani, pumba na molases unaosaidia kuongeza virutubisho muhimu
kwa ukuaji wa mifugo na uzalishaji wa maziwa. Chakula hiki kinaweza kuhifadhiwa
kwa zaidi ya miaka miwili bila kuharibika endapo kitaandaliwa na kuhifadhiwa
kwa usahihi,” alisema Mlamka.
Kwa upande wake mfugaji wa ng’ombe kutoka Kata ya Nzuguni, Mussa Elisha alisema kuwa teknolojia ya silage itakuwa msaada mkubwa kwa wafugaji, hasa wakati wa kiangazi ambapo malisho hupungua kwa kiasi kikubwa.
“Hapo
zamani tulipata wakati mgumu kulisha mifugo kipindi cha ukame, lakini sasa
tukitengeneza silage mapema tunakuwa na uhakika wa chakula kwa muda mrefu. Hii
itachangia mifugo yetu kubaki na afya nzuri na uzalishaji wa maziwa kuendelea
hata wakati wa kiangazi,” alisema Elisha.
Kwa
upande wake mdau wa mifugo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Elineema
Kikumbi alisema kuwa utunzaji wa malisho kupitia teknolojia ya silage ni hatua
muhimu ya kuongeza tija katika sekta ya mifugo na kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
“Dodoma
ni moja ya maeneo yanayokumbwa na ukame mara kwa mara. Wafugaji wanapaswa
kutumia kipindi cha mvua kuandaa akiba ya chakula cha mifugo. Silage ni
suluhisho la kudumu ambalo litasaidia kupunguza vifo vya mifugo, kuongeza
uzalishaji na kuinua kipato cha wafugaji,” alisema Kikumbi.
Wataalamu
wa mifugo wanaendelea kuhimiza wafugaji kuwekeza katika utengenezaji wa silage
ili kuwa na akiba ya malisho mwaka mzima, hatua itakayosaidia kuongeza
uzalishaji wa maziwa na nyama pamoja na kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya
mifugo dhidi ya ukame.
Comments
Post a Comment