City Boys na Royal Village Hotel waunga mkono Timu ya Dodoma Jiji kuelekea SHIMISEMITA

 Na. Mwandishi wetu, DODOMA

KAMPUNI ya uuzaji wa vifaa mbalimbali vya nyumbani na vyombo vya moto City Boys, kwa kushirikiana na Royal Village Hotel, imeendelea kuonesha mshikamano katika kuendeleza michezo kwa kuunga mkono Timu ya Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwakabidhi jezi mbalimbali za michezo kuelekea mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA).



Timu hiyo inayojipanga kushiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu jijini Mbeya, imekabidhiwa bibsi, jezi za mpira wa kikapu pamoja na jezi za mpira wa miguu, hatua inayolenga kuongeza hamasa, morali na ari kwa watumishi wanaoiwakilisha Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofayika ofisini kwake Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya City Boys, Patricia Olomi alisema kuwa wameamua kuunga mkono timu hiyo kwa kutambua nafasi ya michezo katika kujenga afya, mshikamano na kuongeza ufanisi wa watumishi. “Tumeona ni muhimu kuwa sehemu ya maandalizi ya timu yetu kuelekea SHIMISEMITA. Mchango huu ni ishara ya ushirikiano na dhamira yetu ya kuendelea kuunga mkono michezo pamoja na kuwahamasisha watumishi kufanya vizuri ndani na nje ya maeneo yao ya kazi” alisema Olomi.

Kwa upande wake, Meneja wa Royal Village Hotel, Frank Lyimo alisema kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga mahusiano, afya na mshikamano miongoni mwa watumishi, hivyo taasisi binafsi zina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta hiyo. “Tunaamini jezi hizi si mavazi pekee, bali ni sehemu ya kuwapa nguvu na hamasa wachezaji wanapokwenda kuiwakilisha Dodoma. Tunawatakia kila la heri na tunaamini watafanya vizuri huko Mbeya” alisema Lyimo.



Kwa upande wake Afisa Michezo wa Jiji la Dodoma, Neema Kilongola aliwashukuru City Boys na Royal Village Hotel kwa msaada huo, akisema umeongeza morali na kuleta nguvu mpya katika maandalizi ya timu kuelekea mashindano hayo. “Tunawashukuru sana City Boys na Royal Village Hotel kwa kutambua juhudi zetu na kuamua kuwa sehemu ya safari yetu kuelekea SHIMISEMITA. Msaada huu umetupa hamasa kubwa na tunawaahidi kuwa tutapambana kwa nguvu zetu zote na kupata matokeo mazuri” alisema Kilongola.

Kwa sasa, Timu ya Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na maandalizi yake kwa kufanya mazoezi na michezo ya kirafiki, ikiwa na lengo la kuhakikisha inafika jijini Mbeya ikiwa na utimamu kimwili, kiakili na kimchezo kupambana kwa ajili ya heshima ya Jiji la Dodoma.

Comments

Popular Posts

Barabara za Mtaa wa Mbwanga yafunguliwa, Diwani Kerenge aitaja kuwa chachu ya maendeleo

Kanda Namba Tatu yaimarisha ushirikiano na wamiliki wa vituo vya malezi ya watoto Dodoma