Meya Chaula: Kanda za utoaji huduma kusogeza huduma kwa wananchi Dodoma
Na. Mwandishi wetu, MAKUTUPORA
Uanzishwaji wa kanda za
utoaji huduma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni mkakati unaolenga
kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na
kuharakisha maendeleo katika maeneo yote ya jiji.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Dodoma, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alisema kuwa mfumo wa kanda utarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za halmashauri, kupunguza muda wa wananchi kufuata huduma katika makao makuu ya jiji na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji.
Chaula ambae ni Diwani
wa Kata ya Makutupora alisema kuwa kata hiyo ipo katika Kanda Namba Sita hivyo,
wananchi watapata huduma kwa urahisi
zaidi, zikiwemo huduma za usafi wa mazingira, ukusanyaji wa mapato, usimamizi
wa miradi ya maendeleo, pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza
katika maeneo yao kwa wakati.
“Madhumuni ya
uanzishwaji wa kanda hizi ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora
bila kulazimika kusafiri umbali mrefu. Tunataka kuimarisha ushirikiano kati ya
viongozi na wananchi ili maendeleo yafike kwa kila mmoja,” alisema Chaula.
Aidha, aliwataka
wananchi kushirikiana na viongozi wa kanda, kulinda miundombinu ya umma na kushiriki
katika shughuli za maendeleo ili kufanikisha malengo ya kuboresha utoaji wa
huduma ndani ya Jiji la Dodoma.
Kwa upande wake mkazi wa Kata ya Makutupora, Godfrey Kimario alisema kuwa kanda hizo zimewarahisishia wao kupata huduma kwasababu walikuwa wakilazimika kusafirisi umbali mrefu hadi ofisi za jiji kufuata huduma mfano, kulipa tuu leseni na ushuru wa huduma lakini sasa ni rahisi kwasababu kanda ipo karibu nao.
“Tunaishukuru ofisi ya
mkurugenzi kwa kusogeza huduma kupitia kanda maana sasa maafisa biashara wanapita
katika mitaa yetu kwaajili ya kukusanya tozo mbalimbali tofauti na hapo awali
ambapo tulilazimika kwenda hadi jiji” alisema Kimario
Mkutano huo
ulihudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa halmashauri, pamoja
na wananchi wa Kata ya Makurupora ambapo walielezwa utekelezaji wa mfumo wa
kanda utasaidia kupunguza msongamano wa wananchi wanaofuata huduma katika ofisi
za makao makuu ya halmashauri na kuongeza kasi ya utatuzi wa kero za wananchi.
Comments
Post a Comment