Jiji la Dodoma lawapa vijana fursa mikopo ya 10%
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imeendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mikopo ya
asilimia 10, hatua inayowapa nafasi ya kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali
za uzalishaji, ikiwemo viwanda vidogo, utengenezaji wa bidhaa na utunzaji wa
mazingira.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale, Husna Toni mara baada ya kutembelea vikundi vya vijana vinavyofanya shughuli mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alisema
kuwa ziara hiyo imetoa fursa ya kujifunza namna vijana wa Jiji la Dodoma
wanavyotumia mikopo ya asilimia 10 kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia
maendeleo ya jamii. “Vijana wa Dodoma wana uthubutu mkubwa katika shughuli za
uzalishaji, viwanda na utunzaji wa mazingira. Hii inatuonesha kwamba fursa zipo
na vijana wakipewa mitaji na mazingira mazuri wanaweza kujiajiri na kuwa sehemu
muhimu ya maendeleo ya taifa” alisema Toni.
Aliongeza
kuwa vijana wanapaswa kutumia fursa zinazopatikana, hususan mikopo ya asilimia
10 inayotolewa na serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa kuanzisha
shughuli zenye tija na zinazoweza kuwaongezea kipato.
Kwa
upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Estellia
Colman alisema kuwa utekelezaji wa mikopo hiyo umeendelea kuwafungua vijana
macho na kuwafanya kuona kuwa wanaweza kujiajiri na kujenga maisha yao kupitia
mitaji midogo wanayoipata. “Kupitia fursa hizi, tumejifunza kwamba kumbe vijana
wanaweza kujiajiri na kuendesha shughuli za kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia
10. Tunachohitaji ni vijana kuzitambua fursa hizi, kujiunga katika vikundi na
kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa” alisema Colman.
Ziara hiyo imeendelea kuonesha namna uwezeshaji wa vijana kupitia mikopo unavyoweza kuchochea ajira, ujasiriamali, uzalishaji viwandani, usafi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi katika jamii ambapo kikundi kinachojihusisha na utengenezaji wa viatu na kikundi kinachofanya shughuli za uzoaji taka vilitembelewa.
Comments
Post a Comment