Jiji la Dodoma laibuka na zana za upaliliaji, Maonesho ya Nanenane
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imeendelea kung’ara katika Maonesho ya Nanenane kwa kuweka vitu vya kitofauti kama
zana za upaliliaji ambazo zimeundwa na mjasiriamali mdogo wa ndani ya jiji.
Akizungumza na waandishi wa habari
mjasiriamali, Zuberi Nguzo aliyepata fursa ya kuonesha ujuzi katika maonesho
hayo alisema kuwa zana hizo zimeundwa kwa muundo wa ‘power tiller’ ya miguu
mitatu zikiwa katika ubora wa hali ya juu.
“Zana hizi za upaliliaji zinatumia
injini ya guta lakini ina mfumo wa rejeta kama kawaida. Pia ina mfumo wa feni na
upande wa nyuma kuna jembe ambalo hili ndilo linatumika kwa ajili ya
upaliliaji. Katika upaliliaji inatumia mfumo wa matuta kwa maana kwamba inapita
katikati ya mstari na kuweka matuta kwenye mashina ya mahindi kwasababu tairi
zake tumeweka kwa kipimo cha sentimita 62, hiki ni kipimo sahihi kabisa kwa
upana kwa kilimo cha mahindi,” alisema Nguzo.
Alisema kuwa ameamua kubuni zana hizo
kwasababu baadhi ya vifaa vya kuundia vinapatikana kiurahisi mfano, kiti cha
gari, injini ya guta na minyororo ya pikipiki, mambo ambayo yanamfanya kuunda zana
zenye tija katika jamii.
Aliongeza kuwa katika maonesho ya Nanenane kuna vitu ambavyo mwananchi akitembelea katika banda la Jiji la Dodoma atajifunza mengi zaidi na kuweza kupata fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Said Mohamed, mkazi wa
Dodoma alisema kuwa amepata kujifunza mengi katika banda la Jiji la Dodoma,
kikubwa kikiwa ni zana za upaliliaji ambazo zimeundwa kwa mkono na mjasiriamali
wa Dodoma ambazo zinatumika kupapilia mahindi na zinapatikana kiurahisi.
“Maonesho haya ni fursa kwa wakazi wa
Dodoma, nawashauri waje watembelee katika banda hili la jiji kwasababu
watajifunza mengi kama matumizi ya zana za upaliliaji, kilimo cha mahindi,
kilimo cha ngano na kabeji nyekundu ambayo ni nadra sana kuiona katika jamii. Lakini
hapa nimeona na nimeelezwa faida zake,” alisema Mohamed.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea mabanda yake likiwemo banda la mifugo na uvuvi ili kuweza kujifunza masuala mbalimbali.
Comments
Post a Comment