Jiji la Dodoma kuwa kinara ushirikiano na TBS
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imewataka maafisa afya na watumishi wa sekta mbalimbali
kuimarisha ushirikiano na kutumia ipasavyo mafunzo ya matumizi ya mfumo wa
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuongeza ufanisi katika ukaguzi na
usajili wa bidhaa.
Akifungua mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Sebastian Pima alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki kutumia mfumo wa TBS kwa usahihi ili shughuli zote za ukaguzi na usajili ziweze kufanyika kwa ufanisi kupitia mfumo huo.
“Kila
mmoja anatakiwa kushirikiana na wenzake, hizi ni kazi za timu, si za mtu mmoja.
Tunataka Dodoma iwe mfano wa kuigwa nchini katika utekelezaji wa majukumu ya
ushirikiano kati ya TBS na halmashauri, kila afisa atapangiwa malengo ya kila
siku na kila wiki yatakayosaidia kuongeza utendaji na kufikia malengo ya
ukusanyaji wa mapato pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi," alisema Dkt.
Pima.
Aidha,
aliwahimiza washiriki kutumia fursa ya uwepo wa wataalamu wa TBS kuuliza
maswali na kutatua changamoto zote zinazohusu matumizi ya mfumo, akisisitiza
kuwa ushirikiano na kujituma ndiyo msingi wa mafanikio.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa TBS Kanda ya Kati, Donisian Lutahala alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa wa wakaguzi kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya katika kazi.
“Mafunzo
haya yana umuhimu mkubwa kwa sababu tumewafundisha matumizi ya mfumo wa usajili
wa maduka ya bidhaa za chakula na vipodozi unaojulikana kama ‘Online Application System’ (OAS). Mfumo huu utawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, tuna
matumaini kwamba baada ya mafunzo haya, Jiji la Dodoma litaendelea kuimarisha
utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano kati ya TBS na Mamlaka za Serikali za
Mitaa (LGA), na kuwa mfano wa kuigwa kitaifa, sambamba na kaulimbiu yao ya
kwamba 'Dodoma Inapaa',” alisema Lutahala.
Alisema
kuwa mbali na kuwajengea uwezo, mafunzo hayo yamekusudia kuwasaidia wahusika hao
kupiga hatua katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia viwango
vinavyotakiwa.
Comments
Post a Comment