Wafanyabiashara Mnada wa Msalato waahidi kudumisha usafi

Na. Mwandishi wetu, MSALATO

 

Wafanyabiashara na wakazi wa Kata ya Msalato wameiomba serikali kuendeleza kampeni za usafi wa mazingira na kuongeza vifaa pamoja na matunzio ya taka katika maeneo yao ili kuboresha mazingira.

 


Wananchi hao wametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Kampeni Endelevu ya Usafi wa Mazingira uliofanyika katika Mnada wa Msalato, Jiji la Dodoma, yenye kaulimbiu ‘Dodoma Fahari Yetu, Usafi Wajibu Wetu’ uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Senje, Kata ya Msalato, Jackson Chaula alisema kuwa wananchi wamehamasika kushiriki shughuli za usafi bila kujali umri, huku akiwataka kuendeleza utamaduni huo katika maeneo yao ya makazi na biashara kila siku.

 

“Vijana na wazee wote nawaomba tuendelee kuhamasika kufanya usafi kila siku, tuweke vitunzia taka majumbani na kuhakikisha maeneo yetu ya makazi na biashara yanatunzwa vizuri muda wote. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na mazingira salama na yenye afya,” alisema Chaula.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachoma Nyama ya Ng’ombe na Mbuzi katika Mnada huo, Mathias Rafael aliiomba serikali kuongeza matunzio makubwa ya taka katika eneo hilo kutokana na wingi wa taka unaozalishwa eneo hilo na shughuli za biashara.

 


“Tunaiomba serikali ituwekee matunzio makubwa ya taka kwa sababu uzalishaji wa taka hapa ni mkubwa. Tukipata matunzio ya kutosha, itakuwa rahisi kwetu kudhibiti taka na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi muda wote,”alisema Rafael.

 

Nae, mfanyabiashara wa nyama katika Mnada wa Msalato, Irene Mbwambo aliiomba serikali kuhakikisha zoezi la usafi linaendelea kuwa endelevu badala ya kufanyika siku maalumu pekee.

 


“Tunaomba zoezi hili liwe endelevu na lisifanyike Jumamosi hadi Jumamosi pekee. Pia tunaiomba Serikali ituongezee vifaa vya usafi. Nawasihi wafanyabiashara wenzangu tushiriki kikamilifu katika kutunza mazingira yetu, bila kusubiri kukumbushwa,” alisema Mbwambo.


Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, maafisa mbalimbali wa serikali na sekta binafsi pamoja na wananchi.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma Biashara saa 24, usafi saa 24

Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari

Wananchi Dodoma wahimizwa kufanya usafi wa Mazingira kila siku