Prof. Nagu awataka wananchi kuzingatia Lishe bora kukuza Uchumi

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

WANANCHI wametakiwa kuzingatia ulaji bora wa chakula kwa ajili ya kuboresha na kulinda afya kwa kutumia mazao yanayozalishwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili wawe na lishe bora itakayowasaidia kutekeleza majukumu ya kujenga taifa.


Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia masuala ya Afya, Prof. Tumaini Nagu alipotembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Prof. Nagu aliwasisitiza wananchi kuzingatia ulaji wa chakula bora kwa ajili ya afya bora, akisema kuwa mazao yanayozalishwa katika Jiji la Dodoma ni bora na yanamchango mkubwa katika kuboresha lishe. “Niwapongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri mnayoifanya. Pia niwasisitize wananchi hasa vijana kula chakula bora kama tulivyojionea hapa. Mazao yanayozalishwa ni mazao bora kabisa kwa afya. Hivyo, vijana kama kizazi cha baadae wajitahidi kula chakula bora kwa kuzingatia lishe, jambo litakalowasaidia kutekeleza wajibu wao katika kujenga taifa imara” alisema Prof. Nagu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI, Sospeter Mtwale aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri inayofanya katika kuendeleza kilimo na kubuni fursa mbalimbali za maendeleo.



Awali akitoa maelezo kwa viongozi hao walipotembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Clementina Kabaka aliwaelezea juu ya kilimo cha mazao mbalimbali yanayozalishwa jijini hapo, namna ya kuongeza thamani ya mazao pamoja na kuonesha mazao yanayolimwa yakiwepo mazao yanayostawi katika maeneo yenye hali ya hewa ya baridi.

Vilevile, alieleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuelezea fursa za uwekezaji zilizopo, hususan katika sekta ya kilimo na uzalishaji wa mazao yenye tija kwa wananchi.




 

Comments

Popular Posts

Barabara za Mtaa wa Mbwanga yafunguliwa, Diwani Kerenge aitaja kuwa chachu ya maendeleo

Dodoma Jiji yajiandaa Ngoma na Kwaya SHIMISEMITA, 2026

Kanda Namba Tatu yaimarisha ushirikiano na wamiliki wa vituo vya malezi ya watoto Dodoma