Ufugaji wa Ng'ombe aina ya Friesian njia bora ya kuongeza kipato
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamehimizwa
kuwekeza katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa aina ya Friesian kama njia ya kuongeza kipato,
kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa familia kupitia uzalishaji wa
maziwa.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Malecela (Nzuguni), Afisa Mifugo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Frank Mosses alisema kuwa ng’ombe aina ya Friesian ni miongoni mwa mifugo yenye tija kubwa kutokana na uwezo wake wa kuzalisha maziwa kwa wingi endapo atatunzwa kwa lishe bora, maji ya kutosha na usimamizi sahihi.
“Tunatoa elimu kwa wananchi kuhusu
ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa aina ya Friesian, hususan namna ya kuwapatia lishe sahihi,
chanjo, maji safi na mazingira bora ya
kuishi ili kuongeza uzalishaji wa maziwa. Lengo ni kuwasaidia wafugaji kupata
tija na kuboresha maisha yao kupitia ufugaji wenye ufanisi na watija,” alisema Mosses.
Kwa upande wake, Mfugaji kutoka Dodoma, Boniphace Mariwa
alisema kuwa dume la Friesian (Maro) lenye asili ya Afrika Kusini ni ng’ombe bora wa mbegu anayesaidia
kuzalisha ndama wenye ubora na kuboresha uzalishaji wa maziwa.
“Ng’ombe huyu ni mzuri kwa uzalishaji wa mbegu bora zinazosaidia
kupata ndama wenye uwezo mzuri wa uzalishaji wa maziwa. Nawashauri vijana
kujikita katika ufugaji kwa sababu ni shughuli yenye tija na inaweza kuwasaidia
kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi,” alisema Mariwa.
Nae, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, Naamin Mbwambo alisema kuwa ng’ombe wa Friesian anafaa kufugwa katika mfumo wa ufugaji wa ndani (zero grazing) ili kumkinga dhidi ya changamoto za mazingira ikiwemo jua kali na magonjwa, jambo linalosaidia kuongeza uzalishaji mkubwa wa maziwa na kurahisisha usimamizi wa lishe.
“Jike huyu tayari amezaa mara mbili na
huzalisha wastani wa lita 20 za maziwa kwa siku asubuhi 10 na jioni 10, kupitia
mfumo wa ufugaji wa ndani. Mfumo huu unamuwezesha mfugaji kumpatia ng’ombe chakula sahihi, kumtunza vizuri
na kupata uzalishaji mkubwa wa maziwa,”alisema Mbwambo.
Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Ratifa Sibene
mkazi wa Nzuguni alisema kuwa amejifunza umuhimu wa kuwaandalia ng’ombe banda safi, kuwapatia chakula bora
na kuzingatia usafi wakati wa uzalishaji wa maziwa ili kupata maziwa yenye
ubora na salama kwa matumizi.
Hata hivyo, ili kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji, ng’ombe aina ya Friesian anahitaji lishe
bora, huduma za afya na usimamizi mzuri wa mazingira ya ufugaji. Katika
mazingira bora, baadhi ya ng’ombe wa aina hiyo wanaweza kuzalisha hadi lita 45 za maziwa
kwa siku, asubuhi lita 25 na jioni lita 20, kwa kuzingatia lishe na matunzo.
Comments
Post a Comment