Wafanyabiashara Soko la Sabasaba wahimizwa usafi

Na. Mohammed Ramadhani, DODOMA

Wafanyabiashara katika Soko la Sabasaba jijini Dodoma wametakiwa kuendelea kufanya usafi wa mazingira kila siku badala ya kusubiri siku maalum ya usafi, hatua inayolenga kuweka mazingira ya biashara katika hali ya usalama na usafi.



Akizungumza wakati wa zoezi la usafi katika Soko la Sabasaba, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gwantwa Mbwile, alisema kuwa zoezi hilo limeanza tangu Jumatatu na kuendelea hadi Jumamosi, huku akiwataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kufanya usafi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Alisema kuwa kufanya usafi kila siku kunasaidia kupunguza muda na nguvu zinazotumika wakati wa kufanya usafi wa pamoja, kwani taka zinapokusanywa kwa muda mrefu huongezeka na kufanya zoezi kuwa gumu zaidi.

“Wito wangu kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ni kujitahidi kuzoea kufanya usafi kila siku. Hii inarahisisha siku ambayo tunataka kufanya usafi maeneo yetu yanakuwa safi na hatuchukui muda mrefu. Si kusubiri mpaka Jumamosi pekee,” alisema Mbwile.



Kwa upande wake, Katibu wa Soko la Sabasaba, Musa Nyamsuka, alisema kuwa usafi wa mazingira ni muhimu pia katika kujiandaa na msimu wa mvua, za El nino` huku akisisitiza kuwa wafanyabiashara wana wajibu wa kuhakikisha maeneo yao ya biashara yanakuwa safi na salama wakati wote.

Nyamsuka alisema kuwa uongozi wa soko unaendelea kuwakumbusha wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao wa kufanya usafi kila siku ili kuchangia katika kulinda mazingira na kuhakikisha Jiji la Dodoma linaendelea kuwa safi.

Alisema, “kufanya usafi hivi pia tunajiandaa na mvua za El Nino. Mimi kama kiongozi huwa nawakumbusha wafanyabiashara kuwa kufanya usafi ni wajibu wao wa kila siku ili kuweka mazingira ya biashara salama na kuweka Jiji letu la Dodoma likiwa safi”.

Mfanyabiashara wa Soko la Sabasaba, Huseni Mtunya alisema kuwa wafanyabiashara hawafanyi usafi kwa ajili ya siku maalum pekee, bali wamekuwa wakifanya usafi wa maeneo yao kabla ya kuanza shughuli za biashara.

Mtunya alisema utaratibu huo unalenga kuhakikisha wafanyabiashara pamoja na wateja wanapata mazingira salama na rafiki wakati wa kufanya shughuli zao.

“Sisi wafanyabiashara si letu leo tu tunafanya usafi, bali kabla hatujaanza kufungua biashara zetu tunafanya kwanza usafi ili kuweka mazingira salama kwetu sisi na kwa wateja,” alisema Mtunya.



Juhudi hizo zinaendelea kuhamasisha wafanyabiashara na wananchi kufanya usafi kuwa sehemu ya shughuli zao za kila siku, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya biashara, kulinda afya ya jamii na kuunga mkono jitihada za kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi na salama.

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi