Kata ya Ihumwa yaanza usafi kutekeleza agizo la RC Dodoma
Na. Rahma Magona, DODOMA
Kata ya Ihumwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imeanza zoezi la usafi wa mazingira ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa maagizo ya
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ya kuhakikisha wananchi wanaimarisha
usafi wa mazingira na kulinda afya zao.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa Kata ya Ihumwa
kuanza kuhamasisha wananchi kufanya usafi mtaa kwa mtaa kwa kushirikiana na
maafisa afya kutoka Kanda Namba Mbili, huku ukaguzi wa vyoo katika kaya ukiwa
miongoni mwa hatua zinazotekelezwa.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Chang’ombe, Kata ya Ihumwa, Yoram Ndumizi alisema kuwa wamejipanga
vizuri kuhakikisha wananchi wanashiriki katika usafi huku wakifanya ukaguzi wa
vyoo baada ya kubaini baadhi ya kaya kutokuwa na vyoo, hali hiyo inaweza
kuongeza hatari ya mlipuko wa magonjwa kutokana na uwezekano wa mvua nyingi za
El NiƱo.
Ndumizi aliongeza kuwa kwa kushirikiana na maafisa
afya, wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira
na namna unavyoweza kusaidia kuzuia magonjwa ya kuambukiza.
Nae, mkazi wa Kata ya Ihumwa, Onesmo Jonas alisema
kuwa usafi wa mazingira una umuhimu mkubwa katika kulinda afya za wananchi,
akieleza kuwa moja ya faida za kuzingatia usafi ni kuepukana na magonjwa
mbalimbali ikiwemo kipindupindu.
Kata ya Ihumwa imeendelea kuhamasisha wananchi
kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi na kuhakikisha kila kaya inazingatia
usafi wa mazingira pamoja na kuwa na vyoo bora, hatua inayolenga kuzuia
milipuko ya magonjwa na kulinda afya za wananchi.
Comments
Post a Comment