Usafi wa mitaro na njia za maji Kusaidia kujikinga na mafuriko Dodoma Makulu
Na. Amoni Sambulila, DODOMA
Wito umetolewa kwa wananchi kuhakikisha mitaro na njia
za maji zinakuwa safi na wazi wakati wote, ili kuruhusu maji ya mvua kupita kwa
urahisi na kuzuia maji kufurika na kuingia kwenye makazi ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Meneja wa Kanda Namba Nne, Evodius Canisto wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika kata hiyo ambapo aliwataka wananchi kufanya usafi katika maeneo yote yanayoweza kuathiriwa na maji ya mvua.
Evodius alisema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaweza
kusababisha mvua kubwa na kwa nyakati tofauti hivyo wananchi wanapaswa kuchukua
hatua mapema kwa kusafisha mitaro, kuondoa taka na vitu vingine vinavyoweza
kuziba njia za maji.
Aliongeza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila
mwananchi na haupaswi kufanyika wakati wa zoezi maalum pekee bali inapaswa kuwa
sehemu ya maisha ya kila siku ili kulinda afya, usalama na mali za wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shina eneo la Mkalama, Chalesi Jacobo amewataka wananchi kuendelea kushiriki katika usafi wa mazingira akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mitaro inasafishwa mara kwa mara.
Nae, Mwenyekiti wa Shina Namba Mbili, Paulo Ainea
alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwa na utamaduni wa kufanya usafi katika
maeneo yao bila kusubiri kuhamasishwa kwasababu hatua hiyo inaweza kusaidia
kupunguza athari za mafuriko wakati wa mvua zinazotarajiwa kunyesha kwa wingi.
Zoezi hilo limefanyika katika Kata ya Dodoma Makulu
likilenga kuhamasisha wananchi kuimarisha usafi wa mazingira na kujiandaa
mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya
tabianchi.
Comments
Post a Comment