Polisi yaokoa fedha, yaongeza ujenzi wa jengo la ghorofa tatu mradi wa makazi Dodoma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Jeshi la Polisi Wilaya ya Dodoma limepongezwa kwa kufanikiwa kuokoa fedha katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo ya makazi ya askari wa vyeo vya ‘rank and file’ hatua iliyowezesha kuongeza jengo moja la ghorofa tatu licha ya mradi awali kulenga kujenga majengo manane.


 Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi huo eneo la Kutuliza Ghasia Jiji la Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alikipongeza Kikosi Kazi cha Ujenzi cha Jeshi la Polisi kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi na kuwezesha kuokoa fedha za umma.

 

Alisema kuwa hatua hiyo ni mfano wa namna taasisi za serikali, hususan vyombo vya ulinzi na usalama, zinavyoweza kutanguliza uzalendo na matumizi bora ya fedha za umma katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

 

“Kwa hili tunawapongeza kwa dhati. ‘Mme-demonstrate’ kama vyombo vya ulinzi na usalama mkipewa majukumu haya ya nchi, mnatanguliza mbele uzalendo na kuokoa fedha za umma. Hili ni jambo la mfano. Lakini hata kabla ya kupokea zile fedha zote, tayari mmeweza kufanya ‘savings’ na mnaongeza jengo lingine la ziada katika mradi huu,” alisema Alhaj Shekimweri.

 

Akitoa maelezo ya mradi huo, Mhandisi wa Polisi, ASP Gaston Nombo, alisema kuwa awali mradi uliwasilisha andiko la kuomba shilingi bilioni 18.96 lakini hadi sasa shilingi bilioni 16.78 zimepokelewa, huku sehemu ya fedha hizo ikiokolewa na kuwezesha kuanza ujenzi wa jengo moja na kufikisha jumla ya majengo tisa.

 



Alisema kuwa wameongeza pia ujenzi wa uzio wa takribani kilomita 1.4 kuzunguka kambi hiyo, ambao unaendelea kwa hatua mbalimbali, ikiwamo ujenzi wa tofali, upakaji wa plasta na ‘capping’.

 

“Na mradi huu kabla ya ‘variation’ ya bei, jengo moja lilikuwa linagharimu bilioni 2.03. Sasa hivi limeongezeka linaenda na bilioni 2.37. Na andiko lilikuwa tupate bilioni 18. So far tumepata bilioni 16.7, ambazo pia tume-save, tumeanza kujenga ghorofa la tisa,” alisema ASP Nombo.

 

Mradi huo unaendelea kutekelezwa kwa kutumia nguvu kazi ya ndani, huku fedha zilizookolewa zikielekezwa katika kuongeza thamani ya mradi kwa kuanza ujenzi wa jengo la tisa na uzio wa kilomita 1.4, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya makazi na usalama wa askari pamoja na familia zao.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Vijana Dodoma na Iringa Kukutana Kupaza Sauti Dhidi ya Rushwa