Familia 96 kunufaika na mradi wa makazi ya Askari Polisi Dodoma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Jumla ya familia 96 za askari wa vyeo ‘Rank and File’ eneo la kutuliza ghasia wilayani Dodoma zinatarajiwa kunufaika na mradi wa ujenzi wa majengo manane ya ghorofa tatu, unaolenga kuboresha makazi yao kwa kuwapatia nyumba bora, salama na zenye viwango vya kisasa.

 


Mradi huo umefikia asilimia 73 ya utekelezaji, ambapo kila jengo katika mradi huo limepangwa kuhudumia familia 12, huku majengo matano kati ya manane yakiwa yamekamilika na matatu yakiwa katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.

Akizungumza wakati wa kutembelea mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alilipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua waliyofikia, akibainisha kuwa ujenzi huo ni sehemu muhimu ya maboresho ya mazingira ya makazi ya askari.

“Tunawapongeza kwa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huu, na tunawapongeza zaidi kwa kuhakikisha kwamba majengo matano yameshakamilika, huku majengo matatu yakiwa katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Kwa hatua hii, tunaongeza jitihada kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na familia za askari zinapata makazi bora, salama na yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya kisasa,” alisema Alhaj Shekimweri.

Kwa mujibu wa Mhandisi wa Polisi, ASP Gaston Nombo alisema kuwa mradi huo ulianza tarehe 14 Februari, 2024, ukianza na ujenzi wa ghorofa la kwanza, na unatekelezwa kwa kutumia nguvu kazi ya ndani ‘Force Account’ kwa lengo la kupunguza gharama za utekelezaji.

 


Alisema kuwa kila familia itapata nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala, kikiwamo chumba kikuu cha kulala (master bedroom), sebule kubwa, jiko, stoo na choo cha pamoja.

“Mradi huu umetokana na changamoto ya uchakavu mkubwa wa nyumba za makazi ya askari, hali iliyomsukuma Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus M. Wambura, kuwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ombi maalumu la kuboresha makazi ya askari, hususan wenye vyeo vya Rank and File.” alisema ASP Nombo.

Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi 18,962,344,768, ambapo hadi sasa shilingi 16,784,916,000 zimekwishapokelewa kwa ajili ya utekelezaji wake.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Vijana Dodoma na Iringa Kukutana Kupaza Sauti Dhidi ya Rushwa

Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi