Dodoma Jiji FC yajiwinda dhidi ya Namungo dimba la Jamhuri
Na. Amoni Sambulila, DODOMA
Timu ya Dodoma Jiji FC imeendelea na maandalizi
kuelekea mchezo wa raundi ya sita wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya Timu
ya Namungo FC, utakaochezwa leo Ijumaa majira ya saa moja usiku katika Uwanja
wa Jamhuri jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Timu ya Dodoma Jiji FC, Vicent Mashami alisema kuwa timu yake ipo katika hali nzuri baada ya kupata ushindi katika michezo miwili iliyopita, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mwenendo huo wa ushindi.
“Timu ipo vizuri, ambapo mechi mbili zilizopita
tulipata ushindi na hivyo tunahitaji kuwa na mwendelezo wa ushindi. Pia Namungo
ni timu yenye ubora na ushindani, licha ya kupoteza mechi tatu zilizopita,
hivyo tunatambua mchezo huu hautakuwa rahisi,” alisema Mashami.
Kwa upande wake, mchezaji Mwanakibuta David, alisema kuwa
wachezaji wako tayari kupambana katika mchezo huo na kuhakikisha wanaendelea
kupata matokeo mazuri.
“Tunajua mchezo dhidi ya Timu ya Namungo utakuwa na
ushindani, lakini sisi tumejiandaa vizuri na tunahitaji kuendelea na mwenendo
mzuri tuliouanza katika michezo miwili iliyopita,” alisema Mwanakibuta.
Dodoma Jiji FC inaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira
ya kuendeleza matokeo mazuri baada ya kupata ushindi katika michezo miwili
iliyopita, huku Namungo FC ikitafuta kurejea kwenye matokeo mazuri baada ya
kupoteza michezo yake mitatu iliyopita.
Comments
Post a Comment