Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma kuunganishwa na mifumo ya TEHAMA


Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Kituo Kikuu cha Polisi Daraja A kinachojengwa Wilaya ya Dodoma kinatarajiwa kufungwa mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwamo CCTV na chumba maalumu cha udhibiti (control room), kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji wa usalama na udhibiti wa uhalifu mara baada ya kukamilika kwa ujenzi.


 Hatua hiyo ilielezwa wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho pamoja na majengo manane ya ghorofa tatu ya makazi ya askari wa vyeo vya ‘Rank & File’ katika eneo la kutuliza ghasia, Jiji la Dodoma.

 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa chumba maalumu cha ufuatiliaji na udhibiti wa mfumo huo, chenye mazingira rafiki ya kazi na vifaa vya kisasa.

Alisema kuwa matumizi ya CCTV yatasaidia kufuatilia hali ya usalama, kuimarisha usalama barabarani, kudhibiti msongamano wa magari, kupanga doria za kimkakati na kurahisisha upatikanaji wa ushahidi wa matukio.

“Katika dunia ya leo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, hatuna haja ya kuwa na askari wengi wanaozunguka mjini kufanya doria. Kwa mfano huo wa CCTV kamera, hapa unafanya doria kwa kutumia teknolojia, inakupa taarifa,” alisema Alhaj Shekimweri.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Polisi, ASP Gaston Nombo, alisema kuwa teknolojia hiyo imezingatiwa pia katika mradi wa makazi ya askari, ambapo kamera zitawekwa katika maingilio matatu ya eneo hilo.

 


Alisema kuwa kituo hicho kitakuwa na chumba maalumu cha ufuatiliaji na udhibiti, huku mfumo wa CCTV ukitarajiwa kuunganishwa na mtandao wa kamera za ulinzi wa Jiji la Dodoma baada ya kukamilika kwa mradi.

Utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha mazingira ya kazi na makazi ya askari, pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia katika kuimarisha ulinzi na usalama wa Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Vijana Dodoma na Iringa Kukutana Kupaza Sauti Dhidi ya Rushwa