Wazazi wahimizwa kuwapeleka watoto kupata chanjo ya Polio
Na. Josephina Kayugwa, DODOMA
Serikali imejipanga kuhakikisha watoto
wanapatiwa chanjo ya Polio ili kuendelea kuilinda Tanzania dhidi ya ugonjwa
huo, licha ya nchi kutokuwa na mgonjwa wa Polio kwa sasa.
Hayo aliyasema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri katika hafla fupi ya ufunguzi wa kampeni ya utoaji chanjo ya Polio iliyofanyika katika Shule ya Msingi Nkuhungu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa hatua
hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
za kuimarisha afya za watoto nchini, akieleza kuwa watoto wamekuwa sehemu
muhimu ya programu mbalimbali za afya zinazotekelezwa na serikali.
Aliongeza kuwa kama Wilaya ya Dodoma
imepewea lengo la kuwafikia watoto 207,096 katika zoezi hilo, ikiwa ni sehemu
ya jumla ya watoto 1,003,061 katika Mkoa wa Dodoma wanaolengwa katika maeneo
husika.
“Viongozi, watendaji wa serikali, shule, kamati na bodi za shule wamehamasishwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, ikiwamo kuwafikishia wazazi ujumbe kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto kupata chanjo ingawa hatuna changamoto ya mgonjwa wa Polio nchini, ni muhimu kujihami kwa kuwakinga watoto wetu,” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma,
Rosmith Mkoko aliishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo hiyo,
akiwataka wazazi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo.
“Chanjo ni muhimu katika kuwalinda
watoto dhidi ya magonjwa na kwamba wazazi wanapaswa kutumia fursa hii
kuhakikisha watoto wao wanapata kinga. Nawashauri wazazi wawalete watoto wapate
chanjo hizi ili ziweze kuwalinda,” alisema Mkoko.
Zoezi hilo linatarajiwa kuendelea hadi tarehe 30 Agosti, 2026 kwa kushirikisha jamii, hususani wazazi na walezi, ili kuhakikisha watoto wote waliolengwa wanapata chanjo kwa wakati.
Comments
Post a Comment