TARURA Dodoma yatakiwa kukamilisha miradi kwa wakati
Na. Coletha Charles, NZUGUNI
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA)
wametakiwa kukamilisha kwa wakati, miradi ya uboreshaji wa barabara yenye urefu
wa kilomita 3.8 kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha ili iweze kuleta
manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Jiji la Dodoma.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, ikiwa ni sehemu ya hatua za kukabiliana na athari za mvua za El Nino.
Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huyo unapaswa kwenda sambamba na usimamizi madhubuti wa muda, ubora wa kazi na matumizi sahihi ya fedha, ili wananchi wa Jiji la Dodoma wanufaike na miundombinu hiyo kwa muda uliokusudiwa.
“Ninawasihi TARURA kuhakikisha mradi huu unakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, ili wananchi waweze kupata manufaa yaliyokusudiwa. Muhimu ni kuhakikisha fedha zinazotumika katika mradi huu zinatoa thamani halisi kwa wananchi,” alisema Alhaj Shekimweri.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa
TARURA Wilaya ya Dodoma, Mha. Emmanuel Mfinanga alisema kuwa mradi huo inahusisha
Barabara ya Nzuguni kwa Masista yenye urefu wa kilomita 0.5 kwa kiwango cha
lami, pamoja na Nzuguni Makaburini yenye urefu wa kilomita 1.5 kwa kiwango cha
changarawe yenye gharama ya shilingi 694,144,950, huku chanzo cha fedha kikiwa
ni Road Fund Development.
Alisema kuwa TARURA inatekeleza mradi wa Barabara ya Mwangaza yenye urefu wa kilomita 1.1 kwa kiwango cha lami, wenye thamani ya shilingi 1,630,184,137.91, pamoja na Barabara ya Mwangaza Mwambosa yenye urefu wa kilomita 0.7 kwa kiwango cha lami, wenye thamani ya shilingi 880,120,820.12 bila VAT.
“Mradi wa Barabara ya Mwangaza umefikia asilimia 55 ya utekelezaji dhidi ya asilimia 30 ya muda uliotumika, huku Mwangaza Mwambosa ukiwa imefikia asilimia 70 ya utekelezaji dhidi ya asilimia 52.70 ya muda uliotumika,” alisema Mha. Mfinanga.
Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuongeza ubora wa miundombinu ya barabara katika Jiji la Dodoma, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, pamoja na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wakati wa mvua.
MWISHO
Comments
Post a Comment