DC Shekimweri aagiza kampeni maalum ya usafi kukabiliana na El Nino

Na. Coletha Charles, NZUGUNI

TANROADS, TARURA, DUWASA na Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma zimetakiwa kuendesha kampeni maalum ya usafi wa mitaro, makalavati na madaraja katika kipindi cha Mwezi Agosti, Septemba na Oktoba, 2026 ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Nino.



 

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri katika viwanja vya Dkt. John Malecela Kata ya Nzuguni, wakati wa utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua zitakazonyesha kwa kiwango cha juu ya wastani.

 

Alhaj Shekimweri alisema kuwa mvua nyingi huleta athari katika makazi ya watu kutokana na kuzibwa kwa mitaro, makalavati na madaraja, hususan kwa taka na michanga.

 

“TANROADS na TARURA, mnatakiwa kutangulia mkafanye ukaguzi wa hiyo miundombinu ya barabara. Na mimi nitapenda kupewa taarifa ya ukaguzi wenu umebainisha wapi na wapi na kama kuna changamoto kubwa hatua za haraka zichukuliwe. Pengine na sisi tukaongeza nguvu. Ni muhimu sana kushirikiana na serikali za mitaa kwenye jambo hili. Itakapobidi kutumia rasilimali, zitumike kwa uangalifu,” alisema Alhaj Shekimweri.

 

Aidha, alieleza kuwa DUWASA inapaswa kushirikishwa katika maeneo yenye changamoto ya maji na majitaka, akitolea mfano eneo la Kitelela, Nzuguni ambako kumekuwa na changamoto ya mwingiliano wa majitaka na maji safi. Pia, vijana wanaweza kushirikishwa katika kufanya usafi huo, lakini wanapaswa kupewa vifaa vya kazi na vya usalama kulingana na mazingira watakayofanyia kazi.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mha. Filbert Biseko alisema kuwa wakala huo umejipanga kukabiliana na El Nino kwa kusafisha mitaro, kutengeneza barabara na kuandaa mkandarasi wa dharura.

 

“Kwa sehemu kubwa ya mjini hapa, tayari tumeshafanya ‘procurement’ kwa ajili ya kuwapata wakandarasi ambao wataanza kufanya kazi za kusafisha mitaro. Lakini pia, kuna zile barabara ambazo zina changamoto, tayari tumeshapata wakandarasi,” alisema Mha. Biseko.

 

Nae, Meneja wa TARURA Wilaya ya Dodoma, Mha. Emmanuel Mfinanga, alisema kuwa TARURA iko katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi wa kujenga daraja katika eneo la Kitelela, Nzuguni, ambako watoto wamekuwa wakipata changamoto kuvuka wakati wa mvua.

 

“Nakumbuka mwaka jana tulitembelea barabara ya Kitelela, kule Nzuguni. Kuna eneo ambalo watoto walikuwa wanavuka kwa shida, bahati nzuri tuliweka kwenye bajeti na tayari tuko hatua za mwisho kumpata mkandarasi ili akajenge ile daraja na kutengeneza ile barabara,” alisema Mha. Mfinanga.

 

Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Nzuguni, Leonard Ndama alisema kuwa hatua hizo za serikali ni muhimu katika kujiandaa na msimu wa mvua na kuwalinda wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.

 

“Nimefarijika kuona serikali ikichukua hatua mapema. Hii inaonesha kwamba serikali inafanya kazi na inajali usalama wa wananchi, hasa katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua,” alisema Ndama.

 

Utekelezaji wa ukaguzi na usafi wa mitaro, makalavati na madaraja kabla ya msimu wa mvua unatarajiwa kupunguza hatari ya mafuriko na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi. Ushirikiano kati ya TANROADS, TARURA, Serikali za Mitaa, DUWASA na wananchi utakuwa muhimu katika kuhakikisha maandalizi hayo yanafanikiwa.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Vijana watakiwa kujiendeleza nje ya mfumo rasmi

NGOs zatakiwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji Dodoma