DC Shekimweri aagiza utambuzi wa kaya maeneo hatarishi
Na. Coletha Charles, NZUGUNI
Idara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii,
Madiwani, Watendaji wa Kata na Polisi Kata, wameagizwa kushirikiana na mamlaka
nyingine kubaini kaya zinazoishi katika maeneo hatarishi, ikiwemo njia za asili
za maji, yanayoweza kuhatarisha usalama wa maisha na mali za wananchi na
kuzihamasisha kuhamia katika maeneo salama.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri katika Jengo la Utawala la Viwanja vya maonesho ya Nanenane vya Dkt. John Malecela Kata ya Nzuguni, wakati wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kuchukua hatua za kuzuia na kupunguza athari za mvua za El Nino pamoja na mvua zitakazokuwa juu ya wastani.
Alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakijenga
katika njia za asili za maji, hususan wakati wa kiangazi, jambo ambalo linaweza
kuhatarisha maisha na mali wakati wa mvua, ambapo maji hurejea katika mikondo
yake ya kawaida.
“Ujenzi katika maeneo hatarishi hauathiri usalama wa
mtu anayejenga pekee, bali pia huweka familia yake, hususan watoto, katika
mazingira ya hatari. Suala hili linapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia haki na
usalama wa watoto kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009,” alisema
Alhaj Shekimweri.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia
taratibu za ujenzi mijini, ikiwemo mipango ya matumizi ya ardhi na kupata
vibali vya ujenzi kabla ya kuanza ujenzi. “Hatupaswi kusubiri madhara yatokee
ndipo tuchukue hatua. Tunapaswa kuwaelimisha wananchi na kuhakikisha wanatoka
katika maeneo hatarishi na kwenda kuishi katika maeneo salama,” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nzuguni, Leonard
Ndama, alisema kuwa mikakati iliyowekwa na serikali inaweza kusaidia kupunguza
athari za mvua hizo, licha ya kutokuwepo kwa uhakika kuhusu kiwango cha mvua
kitakachonyesha.
“Kwa namna ambavyo mikakati hii imewekwa, nina imani
tunaweza kupunguza kwa kiasi fulani madhara, kwa kuwa hatuwezi kujua kiwango
cha mvua kitakachonyesha wala ukubwa wa madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema
Ndama.
Nae, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya
Dodoma, Insp. Deogratus Peter, alisema kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa
mapema pindi wanapokumbana na changamoto zinazohusiana na maji ili timu za
uokoaji ziweze kufika kwa wakati.
“Ningewaomba watendaji wa mtaa wowote, patakapotokea changamoto,
sio tu Kata ya Nzuguni, wasisite kutuambia kwa kutupigia namba zetu za dharura.
Kuna maji yamezingira au labda kuna bwawa watoto wana shida, basi sisi tuweze
kufika kwa wakati na kutoa msaada huo,” alisema Insp. Peter.
Hatua za mapema za kubaini kaya zinazoishi katika
maeneo hatarishi na kuzielekeza kwenye maeneo salama ni muhimu katika kulinda
maisha na mali.
MWISHO
Comments
Post a Comment