Bwawa kujengwa kudhibiti mafuriko Nzuguni

Na. Coletha Charles, NZUGUNI

Ujenzi wa bwawa kubwa la kuhifadhi maji ya mvua pamoja na mtaro wenye urefu wa zaidi ya kilomita 3.6 umeanza kutekelezwa katika Uwanja wa Maonesho ya Nanenane wa Dkt. John Malecela, hatua inayolenga kudhibiti mafuriko katika eneo la Nzuguni na kuyageuza maji hayo kuwa fursa ya uzalishaji.


 

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo katika Kata ya Nzuguni jijini hapa, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabiri Shekimweri alisema kuwa serikali imejipanga kukabiliana na changamoto ya mafuriko katika eneo hilo, huku ikilenga kutumia maji ya mvua kwa kilimo na uvuvi.

 

Alisema kuwa kwa wastani Dodoma hupokea mvua kati ya milimita 440 na 550 kwa mwaka, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mifumo ya kuvuna na kuhifadhi maji badala ya kuyaacha yapotee.

 

“Bwawa hili litapokea na kuhifadhi maji yanayokusanywa kutoka maeneo yanayozunguka uwanja na hivyo kupunguza hatari ya mafuriko kwa wananchi wa maeneo jirani. Pia mpango huu umezingatia ongezeko la maji linaloweza kutokana na ujenzi wa uwanja wa mpira wa Dodoma pamoja na barabara ya njia sita ya Morogoro, ili miundombinu hiyo isiwe chanzo cha kuongeza hatari ya mafuriko katika eneo la Nzuguni,” alisema Alhaj Shekimweri.

 

Aidha, aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa hatua hiyo, akisema kuwa imefanikiwa kutafsiri maelekezo ya serikali ya kuhakikisha maji ya mvua yanatumika kama fursa ya kuongeza uzalishaji.

 

Akieleza hatua za utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mha. Koyoya Fuko, alisema kuwa bwawa hilo litahifadhi sehemu kubwa ya maji yatakayokusanywa, huku maji machache yatakayozidi yakitolewa kupitia mfumo maalumu wa ‘discharge’ ili kuepusha kuingia kwenye maeneo ya wananchi.

 

Alisema kuwa kazi ya mtaro inatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa Mwezi Oktoba, 2026 huku mfumo wa kutolea maji ukielekezwa kwenye kalavati kubwa ya TARURA mbele ya uwanja na inayounganisha maji na mto.

 

“Mkandarasi tayari ameleta mitambo miwili mikubwa ya kuchimba; mmoja utaanzia upande wa mbele na mwingine utaanzia upande wa chini. Kikubwa ni kwamba maji yote yatakusanywa na hakutakuwa na mtu atakayelalamika katika eneo hili,” alisema Mha. Fuko.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Uwanja wa Nanenane, Mha. David Chitemo, alisema kuwa baada ya kukamilika kwa sehemu kubwa ya barabara za ndani ya uwanja, nguvu sasa imehamishiwa kwenye ujenzi wa mtaro wa nje na bwawa la kuhifadhi maji.

 

Aliongeza kuwa uwanja huo tayari umejengewa takribani kilomita 4.2 za barabara za ndani, huku mtaro mkubwa wa ndani uliokuwa ukisababisha changamoto kwa watu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili ukiwa umekamilishwa kwa sehemu kubwa.

 

“Lengo letu na kazi iliyobaki kubwa sasa hivi ni kumalizia hizo barabara za ndani, lakini kwa sasa nguvu yote tunaihamishia kwenye mtaro wa nje ili tukusanye hayo maji, tuyakusanye kwenye sehemu moja tutaitafsiri kama bwawa, ili tusiwe na madhara kwa wenzetu lakini maji yale yatumike kwa faida,” alisema Mha. Chitemo.

 

Mradi huo unatarajiwa kukamilisha mfumo wa kudhibiti na kuhifadhi maji ya mvua katika Uwanja wa Nanenane, huku serikali ikisisitiza kuwa maji hayo hayatatumika tu kupunguza hatari ya mafuriko, bali pia yatakuwa rasilimali muhimu kwa shughuli za kilimo, uvuvi na uzalishaji mwingine katika eneo hilo.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Vijana watakiwa kujiendeleza nje ya mfumo rasmi

NGOs zatakiwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji Dodoma