DC Shekimweri aagiza kuzingatia usalama maeneo ya uchimbaji madini ujenzi
Na. Coletha Charles, NZUGUNI
Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma imetakiwa
kuandaa orodha ya maeneo yote yaliyotolewa vibali vya uchimbaji wa madini ya
ujenzi, kubaini yaliyo katika matumizi, yaliyokamilisha shughuli za uchimbaji
na yale ambayo hayajarejeshwa katika hali salama.
Agizo hilo limetolewa katika Ofisi ya Utawala viwanja
vya Dkt. John Malecela, Nzuguni na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri katika kikao cha maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El
Nino.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa waendeshaji wa maeneo
hayo wanapaswa kutekeleza mpango wa ‘Environmental Management Plan’ (EMP)
iliyowekwa wakati wa utoaji wa vibali, ikiwemo kusawazisha na kurejesha maeneo
hayo katika hali salama baada ya kumaliza uchimbaji.
“Tupate taarifa wangapi wamezingatia ile EMP na kuweka
maeneo hayo kama inavyotakiwa kwenye EMP na wangapi hawajafanya. Wale ambao
hawajafanya, mnipe orodha lakini muwe tayari mmesha waandikia barua. Nataka
tarehe moja mwezi wa Oktoba, 2026 tupite na Kamati ya Maafa tukakague hayo
maeneo,” alisema Alhaj Shekimweri.
Alisema kuwa waendeshaji ambao watabainika
kutotekeleza masharti ya EMP watachukuliwa hatua za kisheria. Pia, aliwataka maafisa
watendaji wa kata na mitaa kushirikiana na serikali katika kubaini maeneo
yaliyotelekezwa na kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe mapema.
“Nikikuta kuna eneo ambalo halijafanyiwa kazi kwa
mujibu wa EMP, huyo aliyepewa leseni tutamshitaki. Lakini kwa yale maeneo
makubwa ambayo ‘restoration’ yake itachukua muda, yawekwe uzio, milango au
alama za tahadhari ili kuzuia watu kuingia, huku yale madogo yakirejeshwa
katika hali salama kwa haraka,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Wilaya ya Dodoma, Insp. Deogratus Peter, alisema kuwa wazazi na walezi
wanapaswa kuwaelimisha watoto kuepuka maeneo hayo kutokana na hatari iliyopo,
huku watendaji wa kata na mitaa wakitakiwa kuweka alama za tahadhari na
kuendelea kutoa elimu kwa wananchi.
“Ningeomba sana yale maeneo yote kwanza tuweze
kuyatambua. Yale maeneo ambayo wakandarasi wetu tuliwapa zile kandarasi kwa
ajili ya kwenda kuchukua madini ya ujenzi, tujue tunazifanyaje ‘restoration’.
Kama tutashindwa labda kutokana na ‘issues’ za bajeti, basi tuangalie namna ya
kuweza ‘kuzisecure’, kuziwekea ‘cordon tape’,” alisema Insp. Peter.
Kwa hatua hizo, serikali inalenga kuzuia ajali na vifo
vinavyoweza kusababishwa na mashimo ya uchimbaji kujaa maji wakati wa mvua,
huku wamiliki wa maeneo hayo wakitakiwa kutekeleza masharti ya mazingira na
kurejesha maeneo katika hali salama.
MWISHO
Comments
Post a Comment