Dodoma CC Yatwaa Ubingwa wa Mpira wa Mikono SHIMISEMITA, 2026
Na. Leah Mabalwe, MBEYA
Timu ya Mpira wa Mikono ya Wanaume kutoka Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imetwaa ubingwa wa mashindano ya SHIMISEMITA yanayofanyika
jijini Mbeya, baada ya kuicharaza Halmashauri ya Wilaya ya Geita magoli 9-6
katika mchezo wa fainali.
Mchezo huo wa kusisimua ulifanyika katika viwanja vya
Shule ya Sekondari Samora, ambapo timu zote mbili zilionesha ushindani mkubwa
katika kuwania taji hilo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Timu ya
Mpira wa Mikono ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Baraka Muhamed alisema kuwa
mchezo huo ulikuwa mgumu kutokana na timu zote mbili kuwa zilijiandaa vizuri
kwa ajili ya kuwania ubingwa. “Mchezo ulikuwa mgumu kwa sababu pande zote mbili
zilikuwa zimejipanga vizuri kwa ajili ya kuwania ubingwa huu. Tumejituma sana
hadi kufikia hatua hii. Nawashukuru sana wachezaji wote kwa kujituma na kutupa
ushindi huu” alisema Muhamed.
Kwa upande wake, Nahodha wa Timu hiyo, Charles Malima
alisema kuwa wamepata furaha kubwa baada ya kutimiza ahadi waliyompa Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Tuna furaha kubwa sana kwa sababu kile tulichomuahidi
mkurugenzi wetu sasa kimetimia. Pia tunafuraha sana kufika hatua hii, kwa
sababu mwaka jana tulikuwa washindi wa pili, lakini mwaka huu tumetimiza lengo
letu la kuwa mabingwa” alisema Malima.
Nae shabiki wa michezo kutoka jijini Mbeya, Ibrahim Masauti
aliipongeza timu ya Mpira wa Mikono ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
kiwango ilichoonesha katika mashindano hayo, akisema kuwa ushindi wa magoli 9-6
katika mchezo wa fainali si jambo dogo. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma wapo
vizuri. Kushinda magoli 9-6 katika mchezo wa fainali si mchezo. Dodoma Jiji ipo
vizuri. Hivyo, nawashauri halmashauri nyingine zijifunze na kuwekeza zaidi
katika michezo kupitia mfano wa Dodoma Jiji” alisema Masauti.
Ushindi huo unaifanya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
kuandika historia mpya katika mashindano hayo, baada ya kushindwa kutwaa
ubingwa huo mwaka jana na kumaliza katika nafasi ya pili. Mwaka huu, timu hiyo
imefanikiwa kupanda hatua moja zaidi na kuondoka na taji la ubingwa.
Comments
Post a Comment