Wanafunzi Kizota S/M wapatiwa chanjo dhidi ya Polio
Na. Jesca Kipingu, KIZOTA
Wataalamu wa afya kutoka Kituo cha Afya Kizota
wamefika katika Shule ya Msingi Kizota, Kata ya Kizota, Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, kwa ajili ya kutoa chanjo ya Polio kwa watoto wenye umri wa kuanzia
miezi 0 hadi miaka 10, ikiwa ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kuwakinga
watoto dhidi ya ugonjwa huo na madhara yake, ikiwemo ulemavu wa kudumu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Katibu wa Afya katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambaye pia ni Msimamizi wa Kampeni ya Chanjo ya
Polio, Hapiness Kaungya, aliwashukuru wazazi kwa mwitikio mkubwa walioonesha
katika kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo. Alisisitiza kuwa ushiriki wa
wazazi na walezi ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya ugonjwa
wa Polio.
Aidha, Kaungya aliitaka jamii kuendelea kupata na
kuzingatia taarifa sahihi zinazotolewa na wataalamu wa afya ili kuondokana na
dhana potofu kuhusu chanjo. Alisema kuwa ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii
kwa ujumla una mchango mkubwa katika kufanikisha kampeni hiyo na kulinda afya
na ustawi wa watoto.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi Msaidizi II, Naomi
Simon alisema kuwa zoezi la utoaji wa chanjo katika Shule ya Msingi Kizota
limekuwa na mwitikio mzuri, jambo linaloonesha utayari wa wazazi na walezi
kushirikiana na wataalamu wa afya. Aliwaomba wazazi kuendelea kutoa ushirikiano
pale wataalamu wa afya watakapofika katika maeneo ya makazi yao kuwapatia watoto
chanjo.
Nae Kiongozi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW)
wa Kata ya Kizota, Kabla Pima aliwapongeza wazazi wa kata hiyo kwa mwitikio
chanya walioonesha, akieleza kuwa ushirikiano wao umechangia kurahisisha
utekelezaji wa kampeni ya chanjo. Aliwasihi wazazi ambao watoto wao bado
hawajapatiwa chanjo kuhakikisha wanawapeleka kupata huduma hiyo kwa manufaa ya
afya na ustawi wao.
Kwa upande wake Mwalimu wa Afya wa Shule ya Msingi
Kizota, Mwl. Adelmas Mmbando alisema kuwa amefurahi kushiriki katika zoezi hilo
na kuwahimiza wazazi kuondokana na dhana potofu kuhusu chanjo.
Nae mwanafunzi wa Darasa la Nne, Martha Musa, alisema
kuwa wazazi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha watoto wanakuwa na afya njema
na kufikia ndoto zao kwa kuwapatia kinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kuathiri
maisha yao.
Kwa ujumla, zoezi hilo linaendelea kuonesha umuhimu na
ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, shule, wazazi na jamii katika
kuhakikisha kila mtoto mwenye umri kuanzia mwezi 0-miaka 10 anapatiwa chanjo.
Comments
Post a Comment