Diwani Kata ya Miyuji azindua kampeni ya usafi wa Mazingira

Na. Mwandishi wetu, MIYUJI

 

Diwani wa Kata ya Miyuji, Ringo Iringo, amezindua kampeni ya usafi wa mazingira kwa kushirikiana na wataalamu wa Kanda Namba Sita huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.

 


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Iringo amesema kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na changamoto ya uchafu katika maeneo ya makazi na maeneo ya wazi.

 

“Nawasihi wananchi wote tushirikiane katika kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa safi. Usafi ni msingi wa afya bora na maendeleo ya jamii,” amesema Iringo.

 

Amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya usafi mara kwa mara, kutunza maeneo yao na kuepuka kutupa taka hovyo.

 


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyuji Proper, Hawad Mbogela, amewataka wananchi kuunga mkono kampeni hiyo na kuhakikisha usafi unaendelea kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

 

“Tunaomba wananchi wote tushirikiane na viongozi katika kutunza mazingira. Zoezi hili lisibaki kuwa la siku moja; kila mmoja anatakiwa kuhakikisha eneo analoishi na kulizunguka linakuwa safi,” amesema Mbogela.

 

Mbogela amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ni muhimu katika kuhakikisha kampeni ya usafi inakuwa endelevu na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

 

Uzinduzi wa kampeni hiyo umejikita katika kuhamasisha wananchi wa Kata ya Miyuji kuhusu umuhimu wa usafi, utunzaji wa mazingira na uwajibikaji wa pamoja katika kujenga jamii yenye mazingira safi na salama.






Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi

Vijana Dodoma na Iringa Kukutana Kupaza Sauti Dhidi ya Rushwa