TRA yatoa elimu ulipaji kodi kwa NGOs Dodoma
Na. Muhamad Ahmed, DODOMA
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) wilayani Dodoma
yametakiwa kuzingatia wajibu wao wa ulipaji wa kodi na kuhakikisha yanakuwa na
Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha
uwajibikaji na uendeshaji wa shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
Msisitizo huo ulitolewa katika Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Wilaya ya Dodoma leo katika ukumbi wa halmashauri na Afisa Usimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Thomas Lengite wakati akiwasilisha mada isemayo ‘Ulipaji wa Kodi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Upatikanaji wa TIN’.
Alisema kuwa mada hiyo inawapa wadau wa NGOs fursa ya
kupata uelewa kuhusu wajibu wao katika masuala ya kodi, pamoja na umuhimu wa
kuwa na TIN katika kutambulika na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia
taratibu zinazotakiwa.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Moses Mihayo Foundation,
Moses Mihayo alisema kuwa amepata elimu na kufahamu namna ya kuweza kuweka
mipango na mikakati ya kuendeleza taasisi na pia kufahamu namna ya kushughulika
na mifumo pale wanapohitaji huduma.
Jukwaa hilo liliwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu uendeshaji na uendelevu wa NGOs, huku likitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kutafuta njia bora za kuimarisha mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya jamii.
Comments
Post a Comment