Dodoma yasisitiza Elimu nje ya mfumo rasmi
Na. Rahma Magona, DODOMA
Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi
limefikia kilele leo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, huku serikali
ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha fursa za elimu kwa wananchi ambao hawakupata
nafasi ya kusoma katika mfumo rasmi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae ni Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia elimu, Kiduma Mageni alisema kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika uimarishaji wa miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kujifunza.
Alisema kuwa Mkoa wa Dodoma ulipokea zaidi ya shilingi
bilioni 22 kwa ajili ya uimarishaji wa miundombinu ya elimu, hatua inayolenga
kuhakikisha kila mwanafunzi anapata fursa ya kupata elimu katika mfumo rasmi.
Vilevile, wananchi ambao walishindwa kupata elimu
katika mfumo rasmi bado wana nafasi ya kuendelea na masomo kupitia elimu nje ya
mfumo rasmi kwa kutumia miundombinu iliyopo, aliongeza.
Kwa upande wake Witness Isaya alisema kuwa elimu nje ya mfumo rasmi ni muhimu kwa kuwa inatoa nafasi kwa wananchi ambao hawakupata elimu katika mfumo rasmi kuendelea kujifunza na kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.
Maadhimisho hayo yameendelea kusisitiza umuhimu wa
elimu kwa kila mwananchi bila kujali umri au mazingira yake, huku jamii
ikihimizwa kutumia fursa za elimu zinazopatikana ili kuongeza maarifa, ujuzi na
kuchangia maendeleo ya mtu binafsi pamoja na jamii kwa ujumla.
Comments
Post a Comment