Uendelevu wa NGOs wapatiwa msukumo wilayani Dodoma
Na. Amoni Sambulila, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia
Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imeendelea kutoa msukumo kwa mashirika
hayo kuimarisha uendelevu wa shughuli na miradi wanayoitekeleza, ili
kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendelea kuwa na manufaa kwa jamii kwa muda
mrefu.
Akizungumza katika mkutano wa Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ester Erick alisema kuwa uendelevu wa mashirika hayo ni muhimu katika kuhakikisha miradi na huduma zinazotekelezwa kwa ajili ya wananchi zinaendelea kutoa matokeo chanya.
Alisema kuwa katika kipindi cha
utekelezaji, jumla ya miradi 30 ilitekelezwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo
afya, elimu, utunzaji wa mazingira, msaada wa kisheria pamoja na shughuli
zinazohusisha Dawati la Jinsia.
“Jumla ya miradi 30 imetekelezwa
katika maeneo ya afya, elimu, utunzaji wa mazingira, msaada wa sheria na Dawati
la Jinsia, kwa gharama ya shilingi milioni 180.87 na kuwafikia wanufaika
23,632, kati yao wanaume ni 6,001, wanawake ni 7,419 na watoto 10,212” alisema
Erick.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Rise
up Integrity for Human Support (RIHS), John Malale alisema kuwa ushirikiano
kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine ni muhimu
katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta matokeo yenye tija na endelevu
kwa jamii.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa God Bless Network
Foundation, Julius Kilabuka alisema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali
yanapaswa kuendelea kuimarisha uwezo wao wa kiutendaji pamoja na kujenga
ushirikiano madhubuti na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinazotolewa
kwa wananchi zinaendelea kwa ufanisi.
Mkutano huo ulilenga kujadili
utekelezaji wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali, ufuatiliaji wa
miradi inayotekelezwa pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha uendelevu wa
huduma zinazotolewa kwa jamii.
Comments
Post a Comment