Mratibu wa Huduma za Chanjo Atoa Wito kwa Mabalozi Kushiriki Kampeni ya Chanjo ya Polio
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Mratibu wa Huduma za Chanjo wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Victor Kweka amewataka mabalozi kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha
jamii kuhusu umuhimu wa Kampeni ya Chanjo ya Polio, akisisitiza kuwa
ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo
kwa wakati.
Akizungumza na mabalozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri, alisema kuwa wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kila mtoto anapatiwa chanjo kwa wakati, ili kuimarisha ulinzi dhidi ya ugonjwa wa Polio na kulinda kizazi cha sasa na kijacho.
Alisema kuwa mafanikio ya kampeni hiyo yanategemea
ushiriki wa kila mmoja, hususan mabalozi ambao wana nafasi muhimu ya kufikisha
ujumbe wa chanjo katika jamii na kuwahamasisha wazazi kuchukua hatua.
Aliwataka wazazi kutosubiri hadi mtoto aonekane
mgonjwa, bali kuhakikisha anapata chanjo kwa kufuata ratiba iliyowekwa, kwa
kuwa chanjo ni kinga muhimu dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na wataalamu wa afya wakati wa kampeni hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kufikia watoto wote wanaostahili kupata chanjo.
Aliongeza kuwa kila mtoto anayepata chanjo kwa wakati
ni hatua muhimu katika juhudi za kulinda jamii na kujenga kizazi salama dhidi
ya ugonjwa wa Polio.
Comments
Post a Comment