NGO’s Wilaya ya Dodoma wahimizwa ushirikiano
Na. Rahma Magona, DODOMA
Mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani Dodoma
yameaswa kuimarisha ubia, ubunifu na matumizi ya vyanzo vya ndani vya
rasilimali fedha ili kuongeza uendelevu wa shughuli zao na kutoa mchango zaidi
katika maendeleo ya jamii.
Rai hiyo ilitolewa katika mkutano wa Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wilayani Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Joan Mazanda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya Halmashauri ya Jiji Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo, alisema kuwa mashirika
yasiyo ya kiserikali yanachangia katika kujenga ushirikiano na kuibua fikra
endelevu zinazolenga kuimarisha maendeleo ya wananchi. Vilevile, aliongeza kuwa
mashirika hayo yamekuwa yakitekeleza shughuli mbalimbali katika jamii, zikiwemo
afua za afya na mazingira, pamoja na kutoa misaada kwa watoto wanaoishi katika
mazingira magumu.
Kwa upande wake mmoja wa mshiriki kutoka Taasisi ya Binti
Salama, Faith William alisema kuwa mkutano huo umesaidia katika kukutanisha
wadau, kufahamiana, kupata elimu na kufahamu fursa zilizopo.
Mkutano huo umejadili masuala mbalimbali yanayohusu
uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, ubunifu, ujenzi wa ubia pamoja na
upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia vyanzo vya ndani, kwa lengo la
kuimarisha mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya jamii.
Comments
Post a Comment