NGO's Dodoma zahimizwa kuanzisha miradi ya ili kuwa endelevu
Na. Paulo Paulo, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kupitia Jukwaa la
Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), limehimiza mashirika hayo kuanzisha
miradi ya ndani ya kiuchumi ili kujitegemea kifedha badala ya kutegemea
ufadhili wa nje pekee.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Tathimini na Ufuatiliaji kutoka Taasisi ya Reaching the Unreached Tanzania, Eliud Edward alisema kuwa ingawa fursa za kifedha zipo kwa wingi, upatikanaji wake unahitaji jitihada na mbinu za kimkakati kutoka kwa waombaji.
“Upatikanaji wa fedha kwa NGOs ni mchakato
unaohitaji kujitoa kwa dhati. Pesa zipo nyingi sana, ila ili uzipate inategemea
sana wazo la mradi wako,” alisema Edward.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa mashirika
kuhakikisha wazo linalowasilishwa linakuwa endelevu na lenye ubunifu wa ndani
ili kuweza kujitofautisha na waombaji wengine wanawania fursa hizo.
Kwa upande wake Katibu wa Shirika la Afya
Ustawi Foundation, Dominica Kanje aliunga mkono hoja hiyo kwa kusisitiza
umuhimu wa mashirika hayo kujitegemea kiuchumi. “Tumejifunza kwamba sisi kama
mashirika tunatakiwa kuanzisha ubunifu ili kujitegemea, kuanzisha uchumi wetu
binafsi bila kutegemea ufadhili kutoka nje” alisema Kanje.
Jukwaa hilo limewakutanisha wawakilishi mbalimbali wa mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyopo jijini Dodoma, kikiwa na lengo la kujadili uendelevu, ubunifu, na mbinu za upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia vyanzo mbalimbali hasa kipindi hiki dunia inaposhuhudia mabadiliko katika mazingira ya ufadhili, wakati mashirika mengi ya kimataifa yakianza kupunguza au kubadilisha vipaumbele vyao vya kutoa misaada.
Comments
Post a Comment