Timu ya SHIMISEMITA ya Jiji la Dodoma yajipanga kutetea ubingwa

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Kikosi cha Timu ya Watumishi wa Jiji la Dodoma cha Mpira wa Miguu kinaendelea kujifua kwa mazoezi makali kuelekea mashindano ya SHIMISEMITA 2026 yatakayofanyika jijini Mbeya, kikiwa na malengo ya kufanya vizuri na kutwaa ubingwa.



Hayo aliyasema Kocha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Watumishi Jiji la Dodoma, Given Aristides wakati wa bonanza la kimichezo lililozikutanisha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Halmashauri ya Wilaya ya Gairo katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Dodoma, ambapo timu hizo zilipata nafasi ya kupima uwezo wao kabla ya kuingia kambini kwa ajili ya mashindano hayo.

Alisema kuwa ushindani katika SHIMISEMITA unazidi kuongezeka kila mwaka kutokana na halmashauri nyingi kujiandaa kwa umakini, jambo linalowalazimu kuongeza kiwango cha mazoezi na nidhamu ili kufikia malengo waliyojiwekea. “Tunafahamu kuwa SHIMISEMITA ni mashindano yenye ushindani mkubwa, hivyo tunaendelea kujinoa kwa bidii kila siku. Bonanza hili limetupa nafasi ya kupima uwezo wa wachezaji wetu na kubaini maeneo ya kuyafanyia kazi kabla ya kuelekea Mbeya. Tuna imani maandalizi haya yatatuwezesha kufanya vizuri na kuwania ubingwa” alisema Aristides.

Kwa upande wake, Nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Felix Donald alisema kuwa morali ya wachezaji iko juu na kila mmoja ameonesha utayari wa kupambana ili kutetea heshima ya jiji hilo katika mashindano hayo. “Mazoezi yanaendelea vizuri na kila mchezaji anatambua wajibu wake. Sisi ni mabingwa, hivyo tunajua matarajio ya wananchi na viongozi wetu ni makubwa. Tumejipanga kuhakikisha tunarudi na ushindi kama tulivyofanya mwaka jana” alisema Donald.





Mashindano ya SHIMISEMITA 2026 yanatarajiwa kuzikutanisha halmashauri mbalimbali kutoka nchini kote jijini Mbeya, ambapo watumishi wa serikali za mitaa watashindana katika michezo tofauti kwa lengo la kuimarisha afya, mshikamano, ushirikiano na kuibua vipaji vya kimichezo, sambamba na kuwania mataji.

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lashauriwa kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi