Timu ya Jiji la Dodoma yajinoa kuelekea SHIMISEMITA Mbeya, 2026

Na. Mwandishi Wetu, Dodoma

MSAKO wa kutetea ubingwa wa mashindano ya Shirikisho la Michezo la Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) umeanza rasmi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma baada ya watumishi wake kushiriki bonanza la michezo lililozikutanisha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Halmashauri ya Wilaya ya Gairo katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Dodoma.



Bonanza hilo limekuwa sehemu ya maandalizi ya kuelekea mashindano ya SHIMISEMITA yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu jijini Mbeya, ambapo halmashauri mbalimbali nchini zitachuana kuwania ubingwa katika michezo tofauti.

Akizungumza baada ya bonanza hilo, Afisa Michezo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Neema Kilongola alisema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na mechi hizo zimewapa nafasi ya kupima uwezo wa kikosi kabla ya kuelekea Mbeya. “Bonanza hili limetupa nafasi ya kujipima, kurekebisha mapungufu na kuongeza ushindani ndani ya timu. Mwaka jana tulikuwa mabingwa, hivyo mwaka huu tunakwenda Mbeya kutetea ubingwa wetu kwa nguvu zote,” alisema Kilongola.

Kwa upande wake, Mchezaji wa Mpira wa Mkono, Mwidini Mwenda, alisema kuwa morali ya wachezaji iko juu na kila mmoja amedhamiria kupambana ili kuendelea kuipeperusha vema bendera ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Maandalizi yanaendelea vizuri na kila mchezaji anajituma kuhakikisha timu inakuwa katika kiwango bora. Tunafahamu ushindani utakuwa mkubwa, lakini tumejipanga kurudi Dodoma na ushindi kama ilivyokuwa mwaka uliopita,” alisema Mwenda.

Mashindano ya SHIMISEMITA 2026 yanatarajiwa kuzikutanisha halmashauri kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiingia katika mashindano hayo ikiwa na dhamira ya kutetea ubingwa wake.







 

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lashauriwa kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi