Wananchi washauriwa kushirikiana na wataalam wa Afya kufanikisha Kampeni ya Chanjo ya Polio

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Wananchi wametakiwa kushirikiana na wataalamu wa afya katika utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya Polio itakayoanza tarehe 27-30 Agosti, 2026, zoezi hilo litafanyika nyumba kwa nyumba pamoja na katika maeneo yenye mikusanyiko ya watoto na katika vituo vya kutolea huduma za afya.



Akizungumza katika kipindi cha Password ya leo kupitia Manyunyu TV, Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Pima Sebastian alisema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa fursa ya kupata chanjo ya Polio. Aliongeza kuwa timu za afya zitawafikia watoto nyumbani. Maeneo mengine aliyoyataja kuwa yatafikiwa ni katika masoko, shule za msingi, vituo vya kulelea watoto na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watoto.

“Kampeni yetu tutakwenda nyumba kwa nyumba. Yaani mtoto alipo na sisi tutakwenda, tunakwenda na ile ile dhana ya kuhakikisha hakuna mtoto tunamwacha, wananchi hawapaswi kusubiri timu za chanjo ziwafikie majumbani pekee, bali wanapaswa kujitokeza katika vituo vya kutolea huduma za afya watakaposikia zoezi hilo linafanyika katika maeneo yao,” alisema Dkt. Sebastian.

Aidha, alisema kuwa mwitikio wa wananchi katika maandalizi ya kampeni hiyo umekuwa mzuri, akiwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao.

Akiongelea maandalizi, aliyataja kuwa yamehusisha viongozi katika ngazi mbalimbali, kuanzia wilaya, tarafa, kata hadi mitaa, ili kuhakikisha taarifa kuhusu kampeni hiyo inawafikia wananchi wote.

Akiongelea usalama wa chanjo hiyo, aliwahakikishia kuwa chanjo inayotolewa ni salama na kuwataka kuwa na amani na kuendelea kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa afya pale wanapokuwa na maswali.

Kampeni ya chanjo ya Polio inatarajiwa kufanyika tarehe 27-30 Agosti, 2026, huku wataalamu wa afya wakisisitizwa umuhimu wa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata chanjo hiyo kwa ajili ya kuwalinda dhidi ya ugonjwa wa Polio.

 

Comments

Popular Posts

Vijana watakiwa kujiendeleza nje ya mfumo rasmi

NGOs zatakiwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji Dodoma