Dodoma CC Mpira wa Mikono Wanaume yaichakaza Kwimba DC magoli 9–5 na kutinga Nusu Fainali SHIMISEMITA
Na. Mwandishi wetu, MBEYA
Timu ya Mpira wa Mikono ya Wanaume ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imeonesha kiwango bora katika mashindano ya SHIMISEMITA yanayoendelea jijini
Mbeya, baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 9–5 dhidi ya Timu ya Halmashauri
ya Wilaya ya Kwimba katika mchezo wa robo fainali.
Mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkubwa na wenye mvuto mkubwa ulipigwa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Samora, huku Timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikitawala mchezo na kutumia vema nafasi ilizopata hadi kufanikiwa kuondoka na ushindi huo muhimu.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha wa Timu ya
Mpira wa Mikono ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Felician Rocky alisema kuwa ushindi
huo ni matokeo ya maandalizi mazuri, nidhamu na juhudi kubwa zilizofanywa na
wachezaji wake.
“Tumefanya vizuri katika mchezo huu. Wachezaji wameonesha moyo wa
kupambana na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. Ushindi huu umetupa nguvu
na kujiamini zaidi kuelekea mchezo wetu wa nusu fainali” alisema Rocky.
Kwa upande wake, mchezaji wa Timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Baraka Kasasi alisema kuwa kufika hatua ya nusu fainali ni jambo kubwa kwa timu hiyo, lakini hawana mpango wa kuridhika na hatua hiyo.
“Tumefurahi sana kufika hatua hii, lakini bado safari yetu haijaisha.
Tunakwenda kukutana na Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya katika nusu
fainali. Tumejipanga vizuri na tunaamini tutaivuka hatua hiyo na kuelekea
katika hatua inayofuata ambayo ni fainali na tunaendelea kupambana hadi tufikie
malengo yetu ya kuwania ubingwa” alisema Kasasi.
Ushindi wa magoli 9–5 dhidi ya Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba umeongeza matumaini kwa Timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, huku macho ya mashabiki sasa yakielekezwa katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya
Comments
Post a Comment