Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma inayoshiriki SHIMISEMITA yatakiwa kurejea na ushindi

Na. Lulu Luvanda, DODOMA

Timu ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma itakayoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) wametakiwa kulitangaza vema jiji hilo katika michezo kwa kuzingatia nidhamu na misingi ya utumishi wa umma na kurejea na ushindi.

 


Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko wakati wa tukio la kuwaaga wanamichezo hao watakaoshiriki michezo ya SHIMISEMITA jijini Mbeya.

 

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wachezaji hao iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri jijini Dodoma, alisema kuwa mashindano hayo ni fursa ya kulitangaza Jiji la Dodoma kupitia michezo, huku akiwataka wachezaji kuzingatia nidhamu, maadili na misingi ya utumishi wa umma.

 

Alitumia hafla hiyo kumpongeza Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa, Neema Kilongola kwa mchango wake katika kuimarisha michezo ndani ya halmashauri hiyo, akisisitiza kuwa mafanikio ya timu yanaongeza utambulisho wa Dodoma kitaifa.

 


Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa alisema kuwa timu hiyo imejiandaa vizuri na kwamba lengo lao si kushiriki pekee, bali kupigania ushindi. Alisema kuwa maandalizi yamejikita katika kuimarisha maeneo yaliyokuwa na changamoto pamoja na kuongeza uwezo na ushirikiano wa wachezaji.

 

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, mchezaji mwandamizi, Leonard Mkinga alisema kuwa timu imejiandaa vizuri na ina dhamira ya kurejea Dodoma na matokeo mazuri, akitaja nia, maandalizi na nidhamu kuwa nguzo muhimu ya mafanikio.

 

Timu hiyo ina wachezaji 60 inatarajiwa kushiriki mashindano hayo kwa siku 15, ikikabiliana na timu kutoka halmashauri mbalimbali nchini.

Comments

Popular Posts

Dodoma Jiji yajiandaa Ngoma na Kwaya SHIMISEMITA, 2026

Barabara za Mtaa wa Mbwanga yafunguliwa, Diwani Kerenge aitaja kuwa chachu ya maendeleo