Dodoma CC yaangukia msindi wa pili Mpira wa Wavu Wanaume SHIMISEMITA
Na. Leah Mabalwe, MBEYA
TIMU ya Mpira wa Wavu ya Wanaume kutoka Halmashauri ya
Jiji la Dodoma imeibuka mshindi wa pili katika mashindano ya Fainali za
SHIMISEMITA, baada ya kukubali kichapo cha Seti 3-0 kutoka kwa Manispaa ya
Iringa katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari
Samora.
Mchezo huo wa fainali ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku timu zote zikionesha kiwango kizuri cha mchezo na kupambana kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Kocha wa Timu ya Mpira wa Wavu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wanjala Matinya alisema kuwa timu yake ilijiandaa vizuri hadi kufikia hatua ya fainali, lakini pia wapinzani wao walikuwa wamejiandaa ipasavyo na kuweza kupata ushindi.
Kwa upande wake, mchezaji wa Timu ya Mpira wa Wavu, Galucy Kyando alisema kuwa mchezo huo ulikuwa wa ushindani wa hali ya juu kwa sababu kila timu ilihitaji kuondoka na ushindi.
Kyando alisema kuwa licha ya kutwaa nafasi ya pili,
matokeo hayo si mabaya kwa timu yao, kwasababu kufika fainali ni ishara kwamba
timu imeonesha uwezo na ushindani katika mashindano hayo.
“Mpira ulikuwa wa ushindani wa hali ya juu kwa sababu
kila timu ilitaka kuwa ya kwanza. Sisi tumeibuka washindi wa pili, na nafasi
hii si mbaya” alisema Kyando.
Kwa matokeo hayo, Manispaa ya Iringa imeandika
historia ya kutwaa ubingwa wa Mpira wa Wavu wa Wanaume katika Fainali za
SHIMISEMITA, huku Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikijihakikishia nafasi ya pili
baada ya safari nzuri iliyowafikisha katika mchezo wa mwisho wa mashindano.
Comments
Post a Comment