Kata ya Kilimani mbioni kujenga Ofisi kila Mtaa

Na. Emmanuel Charles, KILIMANI

Kata ya Kilimani yatenga kiasi cha shilingi 150,000,000 kwaajili ya ujenzi wa ofisi za serikali za mitaa katika mwaka wa fedha 2025/2026 lengo ikiwa ni kusogeza huduma karibu kwa wananchi.



Haya yalisemwa na Diwani wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko alipokua akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ‘Media Tour’ kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali kuanzia mwaka 2021-2025.

Diwani Mwaluko alisema kuwa Kata ya kilimani ina maeneo ya kutosha kwaajili ya kujenga ofisi za mitaa na wapo wananchi wametoa maeneo yao zijengwe ofisi za mitaa. “Katika yetu tumeazimia kujenga ofisi kwa kila mtaa, lengo letu ni kusogeza huduma kwa jamii. Kuna baadhi ya huduma mwananchi sio lazima aende ofisi ya kata kumfuata afisa mtendaji wa mtaa, ofisi ya mtaa ikiwepo ni rahisi na hatapoteza muda kupata huduma yake. Yupo pia mwananchi mwenye mapenzi mema na maendeleo ya kata, amejitolea eneo lake ijengwe ofisi, tunamshukuru sana” alisema Diwani Mwaluko.

Aliongeza kuwa pamoja na mitaa yote kuwa na maeneo ya kujenga ofisi, mitaa mitatu ina maeneo mazuri na makubwa kwaajili ya ujenzi wa ofisi za mitaa na ana amini Kata ya Kilimani itakuwa kielelezo cha utawala bora. “Niseme kwamba, kata yetu imejipanga kufanya vema eneo la utawala bora na kuboresha huduma kwa wananchi. Naipongeza sana serikali yetu pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa maono na miongozo yao hata sasa tunaamini tutakuwa kata ya mfano kwa kata zilizobaki” aliongeza Diwani Mwaluko.



Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimani, Eliada Msuta alisema kuwa kata yake inafanya vema katika eneo la utawala bora na anaamini kujengwa kwa ofisi za mitaa ufanisi wa kazi utaongezeka maradufu. “Serikali ya awamu ya sita imeweza kuboresha mbinu za utoaji huduma kwa wananchi, tunajitahidi na kujiboresha katika kutoa huduma kama vile usomaji wa taarifa za mapato na matumizi unafanyika kwa wakati, ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya maendeleo unafanyika kwa wakati na utatuzi wa mogogoro unafanyika kwa kina na kuhakikisha amani inapatikana na maisha yanaendelea” alisema Msuta.

Kata ya Kilimani kupitia mpango mkakati huo wa ujenzi wa ofisi za mitaa utaboresha huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya kata na ya Jiji la Dodoma kwa ujumla.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri