Mkopo wa 10% tija kwa maendeleo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu
Na. Aisha Ibrahim, MADUKANI
MIKOPO ya asilimia 10 isiyo na riba kutoka mapato ya
ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa na tija kwa vikundi vya
wajasiriamali na kuwasaidia kukuza kipato na kuinua uchumi katika Kata ya Madukani.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii, Kata ya Madukani, Asha Hussein alipokuwa akiongelea mikopo hiyo na umuhimu wake kwa wananchi wa kata ya madukani.
Alisema kuwa katika kata hiyo kuna jumla ya vikundi 14
vilivyopatiwa mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 273, ambapo wanawake ni
vikundi saba na walipata kiasi cha shilingi milioni 160 na vijana ni vikundi
saba waliopokea kiasi cha shilingi milioni 113.
Alisema kuwa kutokana na mikopo hiyo wanufaika wameweza
kuanzisha shughuli mbalimbali zinazowaingizia kipato na kuweza kujiinua
kiuchumi. “Asilimia kubwa wana vikundi na wameanzisha shughuli zao za
kuwaingizia kipato. Mfano; kuna baadhi yao wanauza nguo, kuna vijana wamefungua
duka la madawa, ufundi wa simu na baadhi ya wakina mama wanajishughulisha na
ushonaji na wamefungua saluni za kike, mbali zaidi wapo wengine wanafanya
shughuli za ufugaji nje ya kata hii” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana cha
Edame, William Frank, kutoka Kata ya Madukani, alisema kikundi hicho
kinajishughulisha na ufundi wa kompyuta, funguo na simu, na kupitia mkopo wa asilimia
10 wameweza kununua vifaa kwaajili ya kuendeshea shughuli zao na kufanikiwa
kuajiri baadhi ya vijana wenye ujuzi katika fani hiyo. “Kupitia mkopo wa asilimia
10 kwa vijana, tumeweza kununua vifaa vya kuendeshea shughuli zetu, mbali zaidi
tumeajiri mpaka vijana wenye taaluma ya ufundi na wanafanya kazi vizuri”
alisema Frank.
Vilevile, aliwaasa vijana kuwa na hali ya uthubutu hata kama hawana mitaji ya kujiajiri waweze kujitoa kufuata taratibu za kupata mikopo hiyo itakayowasaidia kuendesha maisha yao kwasababu haina riba. “Niwaase vijana wenzangu hata kama hawana mtaji wa kuanzisha shughuli yoyote twende tukaombe mikopo hiyo isiyo na riba, hii itasaidia tuweze kujiajiri wenyewe na kuweza kuendesha maisha yetu ya kila siku” alisema Frank.
Nae, mnufaika wa mikopo hiyo, Elizabeth Sebastian, kutoka
Kikundi cha Wanawake cha Amani, alifafanua kuwa kikundi hicho chenye jumla ya
wanachama watano, walifanikiwa kupata mkopo wa kiasi cha shilingi 10,000,000
uliowasaidia kufanya maendeleo na kujikwamua kiuchumi. “Mkopo huu tulioupata
tulifanikiwa kuanzisha mradi wa asali na tulikuwa na mizinga ya nyuki, lakini
kutokana na changamoto tukaamua kufungua duka la nguo na kupitia mkopo
tulioupata mara ya pili duka letu limekuwa kubwa na tumeweza kujikwamua kiuchumi.
Kupitia mikopo hii tunaweza kutunza familia zetu na kutimiza majukumu
mbalimbali ya hapa na pale. Pia tunapambana kuepuka kuwa tegemezi katika jamii
kwasababu maendeleo katika jamii yanakuja kutokana na juhudi za kupambana”
alisema Sebastian.
MWISHO
Comments
Post a Comment